Klabu ya Yanga imesema itatangaza chanzo cha fedha za ujenzi wa Uwanja wa Kaunda unaotarajiwa kugharimu sh.bilioni 43 Aprili 17.
Aidha, Yanga imesema siku hiyo pia ndiyo
itachagua mchoro wa uwanja inaopendelea miongoni mwa mitatu
iliyowasilishwa kwake na kampuni ya Beijing Construction ya China,
iliyoteuliwa kujenga uwanja huo.
Kampuni hiyo ya China ilikabidhi michoro
hiyo Alhamisi na kamati ya utendaji ya Yanga itakutana Aprili 17 kwa
ajili ya kupitia michoro na mapendekezo ya kampuni hiyo.
Afisa
Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto amesema mara baada ya kikao hicho
cha kamati ya utendaji ndipo chanzo cha fedha zitakazotumika katika
ujenzi wa uwanja huo kitakapoelezwa.
"Uongozi uliweka kalenda katika mchakato
wa ujenzi wa uwanja, hivyo baada ya kupokea michoro ya uwanja kwa sasa
tunasubiri kikao cha kamati ya utendaji ambacho kitapitia michoro na
kutoa mapendekezo kwa kampuni ya ujenzi ya Beijing," alisema Kizunguto.
Aidha, alisema kuwa uongozi wa klabu hiyo
umejipanga na una nia ya dhati ya kufanikisha ujenzi huo na tayari
unafahamu njia ya kupata fedha za ujenzi wa uwanja huo ambazo ndizo
zitatangazwa baada ya kikao hicho.
Alisema kwa mujibu ya kalenda ya klabu hiyo ya ujenzi, uwanja huo unategemea kuanza kujengwa mwishoni mwa mwezi ujao.
Si mara ya kwanza kwa klabu ya Yanga
kutangaza maboresho kwa kujenga upya Uwanja wa Kaunda ambao licha ya
uchakavu, upo katika eneo ambalo hukumbwa na mafuriko ya maji yatokanayo
na mvua za masika kila mwaka kwenye bonde la mto Msimbazi.
Ni mara ya kwanza, hata hivyo, kwa uongozi
wa timu hiyo kuingia mkataba na kampuni ya uhakika ya ujenzi wa majengo
makubwa kama iivyo Beijing Construction.
Beijing Construction ndiyo iliyojenga
Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kuketisha chini kidogo ya watazamaji
60,000 na imeshatoa kwa Yanga michoro mitatu ya viwanja vyenye kuingiza
watazamaji 15,000 waliokaa.
No comments:
Post a Comment