Baada ya serikali kutangaza juzi kuwa imeifuta katiba mpya ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kutaka itumike kwa katiba ya zamani
iliyopitishwa mwaka 2006, Tanzania imejiweka katika hatari zaidi ya
kufungiwa kuliko ilivyowahi kutokea wakati wowote kwani uamuzi huo
unaweza kupingana moja kwa moja na kanuni za Shirikisho la Soka la
Kimataifa (FIFA), .
Mmoja wa wanasheria maarufu ambao
pia hujihusisha na shughuli za soka, amesema kwamba serikali ilipaswa
kuwa na subira baada ya kuwapo na taarifa za FIFA kutuma ujumbe wake
nchini kwa nia ya kutatua mgogoro uliopo hivi sasa kuhusiana na
kuenguliwa kwa baadhi ya watu wanaowania uongozi TFF, wakiwamo Jamal
Malinzi anayewania urais na Michael Wambura (makamu wa rais).
Mwanasheria huyo alisema kuwa baada ya serikali kufuta katiba mpya,
inamaanisha kwamba sasa mambo mengi yaliyofanyika kwa kufuata
marekebisho ya katiba mpya yatakuwa yamevurugika na baadhi ya wajumbe
watapoteza sifa za kuingia kwenye mkutano mkuu.
Aliongeza vilevile kuwa, nafasi kama za Makamu wa Kwanza na wa Pili
wa Rais wa TFF hazimo katika katiba mpya na badala yake, kuna makamu
mmoja tu, tofauti na katiba ya TFF iliyoamrishwa kutumika sasa ya mwaka
2006. Kwa maelekezo ya FIFA, makamu wa rais wa shirikisho (TFF)
hawapaswi kuwa wawili bali mmoja.
"Wangesubiri FIFA kuja kutatua tatizo hilo na ndipo serikali
ichukua maamuzi yake… na maana ya FIFA kutuma ujumbe ni kulenga
kusuluhisha tatizo," alisema mwanasheria huyo.
Serikali iliamua kufuta katiba ya TFF kutokana na kile ilichoeleza
kuwa ni kugundua kwamba marekebisho mapya ya katiba hiyo hayakufuata
kanuni na sheria zilizowekwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambazo
ni halali nchini na zimetungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella
Mukangara, alisema juzi kwamba kabla ya kusajiliwa kwa katiba mpya, TFF
ilipaswa kujaza fomu za aina nne tofauti na endapo ingekuwa imekubaliwa,
ingejibiwa kwa kupewa fomu namba 11 lakini hatua zote hizo
hazikufuatwa.
Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana Jumamosi jijini Dar es Salaam kujadili uamuzi huo wa serikali.
Kwa mujibu wa kanuni za FIFA, ni marufuku kwa serikali na mamlaka
zake nyingine kuingilia masuala ya soka na hilo likibainika, shirikisho
hilo (FIFA) hutoa muda maalum wa kusaka suluhu na ikishindikana,
hufungia nchi husika kama ilivyowahi kutokea nchini Kenya.
No comments:
Post a Comment