HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

9 June 2013

Ravia Idarous Faina (42) NDIYE MBOSI MPYA ZFA

 
CHAMA cha Soka Zanzibar, kimepata Rais mpya kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika leo katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
 
Aliyefanikiwa kukalia kiti hicho, ni Ravia Idarous Faina (42), aliyewabwaga wapinzani wake wawili, kwa kuzoa kura 37 kati ya 53 zilizopigwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa ZFA. Abdallah Juma Mohammed, Mwanasheria wa chama hicho, yeye alipata kura 16, huku mwanafunzi anayetarajia kuhitimu digrii ya sheria katika Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu , Rajab Ali Rajab akishindwa kupata hata kura moja.
 
Uchaguzi huo uliitishwa kufuatia kujiuzulu kwa Amani Ibrahim Makungu mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, baada ya kukiongoza chama hicho kwa miezi saba tu.
 
Makungu pia alichukua nafasi hiyo kupitia uchaguzi mdogo uliofanyika Juni 30, 2012, baada ya kuachia ngazi kwa Ali Ferej Tamim, aliyekaa madarakani kwa zaidi ya miongo miwili.
 
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho Gulam Abdallah Rashid, Rais huyo mpya aliwashukuru wote waliomchagua na waliomnyima kura, na kusema ushindi huo ni wa kila anayelitakia mema ZFA na soka la Zanzibar.
 
, kila uchaguzi unakuwa na mambo yake, pamoja na wagombea kubebwa na watu wanaowaunga mkono, lakini mwisho mshindi anakuwa mmoja, hivyo wapiga kura wanapaswa kuvunja kambi zao ili kuimarisha chama na kufanya kazi kwa matakwa ya Wazanzibari.
 
Aliahidi kuongoza kwa kufuata katiba na kanuni zinazotawala mpira wa miguu Zanzibar , na kusema hatakaribisha nafasi ya uongozi au utendaji isiyotajwa ndani ya katiba.
 
Aidha, alisema kwa wakati wote akiwa madarakani, atahakikisha chama kinakuwa na sauti ya pamoja na kuvunja mgawanyiko kati ya Unguja na Pemba ( UFA na PFA) yaani Unguja Football Association na Pemba Football Association kama wengi walivyoanza kubatiza.
 
Mpinzani wa karibu wa Ravia, Abdallah Juma Mohammed alimpongeza mshindi huyo na kusema amekubali matokeo na namna Kamati ya Uchaguzi ilivyoendesha zoezi hilo . “Uchaguzi ni mchezo wa kubahatisha, yawezekana wapiga kura wamevutiwa zaidi na sera za mgombea mwenzangu na hivyo kumpigia kura nyingi. Hata hivyo ninaahidi kumsaidia kwa ushauri na lolote atakalotaka kwa manufaa ya soka letu,” alieleza.
 
Naye Rajab Ali Rajab ambaye hakuambulia kura yoyote, alikiri kuwa uchaguzi umefanyika vizuri, ingawa alionesha wasiwasi kuwa huenda wapiga kura ZFA wanaangalia zaidi sura na umaarufu, na sio sera za wagombea.
 
Alisema idadi ndogo ya wapiga kura, inachangia kushawishi kurubuniwa, na hivyo mshindi kupatikana kwa namna anavyokunjua mkono wake.
 
Mwenyeikiti wa Kamati ya Uchaguzi Gulam Abdallah Rashid, aliishauri ZFA kuwa makini katika maandalizi, na kuepuka kasoro zinazosababisha usumbufu ikiwemo kuchelewa kuipa kamati yake taarifa muhimu.
 
Ravia anakuwa Rais wa tatu ndani ya kipindi kimoja cha uchaguzi ambacho uongozi wake hudumu wa miaka minne, akitanguliwa na Ali Ferej Tamim na Amani Ibrahim Makungu waliobwaga manyanga kwa sababu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers