HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

27 September 2013

MAMBO YANGONGA MWAMBA TFF

 
 
Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetangaza hukumu ya mashauri nane yaliyowasilishwa mbele yake kwa kumsafisha mlalamikiwa mmoja, kutowaadhibu zaidi washtakiwa sita na kuahirisha kusikiliza shauri moja baada ya mlalamikiwa kutokuwepo.

Riziki Juma Majala, ambaye ni Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) ndiye pekee aliyesafishwa na Kamati ya Maadili dhidi ya mashtaka ya kutoa kauli zilizosababisha kufunguliwa kwa kesi dhidi ya TFF.

Vilevile Kamati imesita kuwachukulia hatua Shafii Dauda, Nazarius Kilungeja, Wilfred Kidao, Omar Isaak Abdulkadir na Kamwanga Tambwe kutokana na kuridhika kuwa wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi, hivyo hawawezi kuadhibiwa mara mbili.

Pia imesema haiwezi kumuadhibu Richard Julius Rukambura, aliyeshtakiwa kwa kukiuka Katiba ya TFF kwa kosa la kufungua kesi mahakamani, baada ya kubaini kuwa si mwanafamilia wa TFF kutokana na kuenguliwa kwenye uchaguzi.

Hoja hiyo pia ilitumika kutomchukulia hatua Dauda na mwamuzi wa zamani Omar Abdulkadir kwa hoja kuwa walipoteza sifa za kuwa wanafamilia wa TFF baada ya kuenguliwa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi.

Shauri la Omary Mussa Mkwaruro la tuhuma za kutumia cheti cha elimu kisichotambuliwa na mamlaka husika, limeahirishwa kutokana na Mlalamikiwa kutowasilisha utetezi wake, hivyo Kamati imeagiza Sekretarieti kuwasiliana naye ili awasilishe maelezo yake.

Watu hao walifikishwa mbele ya Kamati ya Maadili baada ya kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa TFF na baada ya usaili walibainika kuwa na matatizo ya kimaadili, hivyo ili iamue juu ya hadhi yao katika familia ya mpira wa miguu kwa kuwachukulia hatua au kuwaweka huru.
Katika hukumu iliyotolewa leo (Septemba 26 mwaka huu), Kamati ya Maadili imeeleza kuwa Majala hakiuka Kanuni za Maadili kwa kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na TFF vinaonyesha kuwa klabu ya Kiluvya United imesajiliwa na Serikali na vyama wanachama wa TFF.

Kuhusu Rukambura, ambaye alilalamikiwa kwa kuipeleka TFF kwenye mahakama ya kiraia, hivyo kukiuka Kanuni ya 73 (3) (b) ya Kanuni za Maadili, Kamati imesema ushahidi uliowasilishwa na TFF hauonyeshi kama mgombea ni mwanafamilia wa TFF; alishaondolewa katika uchaguzi na hivyo si kati ya wagombea na hivyo mikono ya Kamati kufungwa kwa mujibu wa kanuni ya pili ya Kanuni za Maadili.

Kamati pia imeeleza kuwa Kanuni ya 73 (3) ambayo ingepaswa kutumika kumchukulia hatua, chimbuko lake ni Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF ambayo inawalenga wanachama tu na hivyo kuamua kuwa malalamiko hayo hayana mashiko na kwani Rukambura alishapoteza sifa za kuwa mwanafamilia na hivyo kushindwa kumchukulia hatua.

Kidao alishtakiwa kwa kosa la kumiliki nyaraka za Kamati ya Utendaji kinyume na taratibu na pia kuwasilisha malalamiko yake Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) bila ya kufuata taratibu, lakini Kamati imesema kwa vile mlalamikiwa ameenguliwa kwenye uchaguzi, anatumikia adhabu ya kinidhamu na hivyo haiwezi kumuadhibu mara mbili.

Kuhusu Shafii Dauda, Kamati imesema malalamiko dhidi yake hayana mashiko kwa kuwa si mwanafamilia wa TFF na kwamba lalamiko dhidi yake linatupiliwa mbali kwa kuwa tayari ameshaondolewa kwenye uchaguzi kutokana na kosa la kinidhamu.

Kamati iliona hakukuwa na haja ya kushughulikia mashauri dhidi ya Nazarius Kilungeja, ambaye alishtakiwa kwa kukaidi maagizo ya vyombo halali vya TFF, na Kamwanga Tambwe kwa kuwa tayari wawili hao wanatumikia adhabu ya kufungiwa na Kamati ya Nidhamu.

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers