Michael
Wambura aliomba uongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara
(FAM) katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana. Kamati ya Uchaguzi
ya TFF iliondoa jina lake kwa kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo.
Wambura
hakuridhika na uamuzi huo akapeleka shauri lake Kamati ya Nidhamu ya
TFF. Kamati hiyo katika uamuzi wake ilisema haina mamlaka ya
kushughulikia shauri hilo. Baadaye Wambura alikata rufani katika Kamati
ya Rufani ya TFF ambayo ilimpa haki ya kugombea.
Kutokana
na mkanganyiko huo wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwa na uamuzi wa
mwisho katika masuala ya uchaguzi ya wanachama wa TFF, na uamuzi wa
Kamati ya Rufani kuhusu uchaguzi wa mwanachama wa TFF, Sekretarieti ya
TFF iliomba mwongozo wa kisheria kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi
za Wachezaji.
Kwa
vile Kamati hizo mbili (Uchaguzi na Rufani) haziko katika mtiririko wa
moja kwa moja wa utoaji maamuzi, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji iliishauri Sekretarieti ya TFF kuliandikia Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ili kupata muongozo juu ya suala
hilo.
Katika
muongozo wake, FIFA ilitoa maoni kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF
chombo cha mwisho cha rufani katika masuala ya uchaguzi kwa wanachama wa
TFF ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Hata hivyo, FIFA ilishauri kuwa si
vizuri chombo kimoja kikawa msimamizi wa uchaguzi, na chenyewe tena
ndiyo kiwe cha mwisho katika uamuzi kwenye uchaguzi husika.
Hivyo,
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji imetoa mapendekezo
mawili kwenda Kamati ya Utendaji kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ili
kiwepo chombo kingine cha rufani pale mgombea anapopinga uamuzi wa
Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Mapendekezo
hayo ni; Iundwe Kamati ambayo itakuwa inasikiliza rufani zote
zinazotokana na uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, hivyo
Kamati ya Uchaguzi ya TFF isiwe chombo cha mwisho cha uamuzi kwa rufani
zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF.
AU.
Rufani zote zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF zisikilizwe na
Kamati ya Rufani ya TFF. Kwa maana hiyo Kamati ya Rufani ya TFF ndiyo
kiwe chombo cha mwisho kwa wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi ya TFF kuwasilisha malalamiko yao.
No comments:
Post a Comment