FRANCIS Cheka ‘SMG’ wa Morogoro, ameendeleza ubabe dhidi ya mabondia wa Dar es Salaam, baada ya kumtandika kwa Technical Knockout (TKO), raundi ya sita Karama Nyilawila na kutwaa ubingwa wa UBO uzito wa Middle, kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba, Dar es Salaam muda mchache uliopita katika pambano ambalo lilipangwa kuwa la raundi 12.
Karama aliingia kwa kasi katika pambano hilo na kutumia nguvu nyingi kumshambulia Cheka, ambaye alikuwa mtulivu akipangua na kukwepa ngumi nyingi za mpinzani wake huyo.
Kuna wakati kwa kasi ya Karama na namna Cheka alivyokuwa akirudi nyuma kwa makonde ya kusukumwa na mpinzani wake, wengi waliamini labda siku ya kuzima ubabe wa bondia wa Morogoro imewadia.
Hata hivyo, raundi tatu tu zilitosha kumaliza cheche za Karama na tofauti na randi za awali alivyokuwa akirudi kwenye kona yake alikuwa akisimama, lakini baada ya raundi hiyo, aliomba kiti, wakati mpinzani wake aliendelea kusimama.
Kuanzia raundi ya nne, ilionekana dhahiri Karama ameishiwa nguvu na pumzi na ndipo Cheka alipoanza kumshughulikia.
Katika raundi ya sita, Cheka aliingia kwa kasi na akafanikiwa kumtandika mpinzani wake upper-cut na hook iliyomkalisha chini. Alihesabiwa hadi saba, akajikokota kuinuka, lakini mishipa ya kichwa ilikuwa bado haiwasiliani hivyo akaamua kunyoosha mikono yake miwili juu, maana yake; amesalimu amri.
Hapo ndipo shangwe zilipoibuka katika ukumbi wa PTA, watu wakimpongeza Cheka kuendeleza ubabe wake.
No comments:
Post a Comment