Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imepangwa kucheza na Uganda (The
Cranes) katika raundi ya kwanza ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika Afrika
Kusini mwaka 2014.
Kwa
mujibu wa ratiba iliyopangwa jana (Septemba 7 mwaka huu) makao makuu ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) jijini Cairo, Tanzania
imeingia moja kwa moja raundi ya kwanza ambapo itacheza na Uganda.
Mechi
ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kati ya Juni
21,22 na 23, 2013 wakati ya marudiano itachezwa katika Uwanja wa Mandela ulioko
Namboole jijini Kampala kati ya Julai 5,6 na 7, 2013.
Nchi
38 zinashiriki katika mechi hizo za mchujo ambapo nyingine zitaanzia
raundi ya awali itakayochezwa kati ya Novemba 30 na Desemba 1 na 2 mwaka
huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Desemba 14,15 na 16
mwaka huu.
Ratiba
imepangwa kwa makundi ya kanda ambapo jumla ya timu 16 ndizo
zitakazocheza fainali hizo nchini Afrika Kusini. Kanda hizo ni Kaskazini
itakayopeleka timu mbili katika fainali, Magharibi A (timu mbili),
Magharibi B (timu tatu), Kati (timu tatu), Kati Mashariki (timu tatu),
Kusini (timu tatu akiwemo mwenyeji Afrika Kusini).
Kwa upande wa kanda ya Tanzania (Kati Mashariki), timu zinazoanzia raundi ya awali ni Burundi, Eritrea, Ethiopia na Kenya.
Fainali
za Kwanza za CHAN zilifanyika mwaka 2009 nchini Ivory Coast ambapo
Tanzania ilishiriki huku Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ikiibuka
bingwa.
Fainali za Pili zilichezwa mwaka 2011 nchini Sudan ambapo
Tunisia ilitwaa ubingwa. Fainali za Kwanza zilishirikisha timu nane
kabla ya kuongezwa hadi 16 za sasa.
No comments:
Post a Comment