Zaidi ya wanariadha 200 wamethibitisha kushiriki tamasha la mwaka huu la michezo la Karatu itakalofikia kilele chake Desemba 22.
Tamasha hilo la kila mwaka tayari limekwishaanza, ambapo mechi za mpira wa miguu na michezo mingine zinaendelea na zinatarajia kufikia tamati Desemba 21 kabla ya washindi kukabidhiwa zawadi zao Desemba 22, siku ya ufungaji wa tamasha hilo.
Mratibu wa tamasha hilo, Meta Petro amesema kuwa wanariadha zaidi ya 200 wameshajiandikisha kuahiriki tamasha hilo, 160 wakiwa ni wanaume.
Amesema kuwa wanaume na wanawake watachuana katika mbio za Km 10 wakati watoto wenye umri chini ya miaka 14 watapimana ubavu katika mbio za Kilometa tano.
Petro alizitaja baadhi ya timu zilizothibitisha kuleta wanariadha wake katika tamasha hilo kuwa ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Majira Athletics Club, Hakika Wining Spirit, Guang ya Mbulu, Rift Valley ya Karatu na klabu ya Babati huku Zanzibar utawakilishwa na klabu ya Mukijope.
Mbali na riadha ambayo itafanyika siku ya kilele cha tamasha hilo Desemba 22, mchezo mwingine ni mbio za baiskeli ambao washiriki watachuana katika mbio za Km 60.
Amesema kuwa tayari waendesha baiskeli 33 wameshajiandikisha kushiriki katika mbio hizo na kwa upande wa mpira wa wavu, timu ambazo tayari zimethibitisha kushiriki ni JKT Arusha, Mbulu KKKT, Mbulu Wahame na Karatu Gypsum, ambao wataanza mbio za kusaka ubingwa Desemba 20.
Amesema tamasha hilo ambalo hadi sasa lina zaidi ya miaka 10 tangu lianzishwe lina lengo la kuibua na kuviendeleza vipaji mbalimbali.
“Tuna mpango wa kuwasaka kina Filbert Bayi wapya watakaochukua nafasi ya bingwa wazamani wa dunia wa mbio za M 1,500. Bayi ni mzaliwa wa Karatu na kupitia taasisi yake ya Filbert Bayi Foundation na Olympic Solidarity pamoja na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), amekuwa akiendesha tamasha hili la michezo na utamaduni kila mwaka ili kuibua vipaji vipya na hali ya kupenda michezo kwa vijana wa Karatu na Tanzania kwa ujumla,”.
No comments:
Post a Comment