*Yawezekana hili ni swali ambalo wengi watajiuliza au wachache watatamani kupata majibu yake haraka.
Hata hivyo, itoshe tu kwa wenye macho na mwono wa mbali kujua ni nini
kinachofuata baada ya yote yaliyofanyika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Nianze tu kwa kuwasimulia au kuwakumbusha kisa cha miaka iliyopita
kilichomtokea bwana mmoja kutoka Mashariki ya Kati (barani Asia}.
Huyo na bosi wake walikuwa marafiki wakubwa na waliandamana kila
walikokwenda. Wakatokea kuwa watu wa kupigiwa mfano kwenye kusaidiana,
ili waigwe.
Hakika hakuna hata aliyeota kwamba ingefika siku wakawa maadui
wakubwa katika maisha yao. Kisa hiki ni kirefu sana, lakini itoshe
kufasiri ule usemi maarufu; ‘adui mkubwa ni rafiki yako na rafiki yako
ndiye adui yako mkubwa msipokuwa makini’.
Yataka upana na upeo wa jicho la tatu kuona kile ambacho kitatokea
baada ya miaka minane ya TFF dhidi ya simba kutoka milima ya nyika.
Leodegar Chila Tenga ni mmoja wa watu ambao kwa hakika naweza kusema
wamelipa heshima soka la Tanzania, kwa maana ya kurudisha mfumo na
muundo wa utawala unaotakiwa.
Si siri kwamba amelipa shirikisho hilo taswira nzuri na kuleta hadhi
na heshima ya ofisi yenye dhamana ya kandanda nchini Tanzania.
Kadhalika amelifanya shirikisho hilo kuwa na hadhi ya kukubalika na kukopesheka kibiashara ndani na nje ya nchi.
Imani ambayo Tenga na wasaidizi wake, kwa maana ya kamati zote pamoja
na sekretarieti mbili alizofanya nazo kazi – kuanzia ya akina Frederick
Mwakalebela hadi ya sasa ya akina Angetile Osiah ni kielelezo cha
ufanisi wa kazi chini ya Tenga.
Dhamira kuu aliyoingia nayo TFF ni kuona shirikisho hilo linakuwa
chombo imara na kurudisha mfumo wa soka unaoeleweka, jambo
alilofanikisha kwa zaidi ya asilimia 75. Kashindwa kwenye baadhi ya
nyanja.
Kuna ambao bado hawataona au hawataki kuona alichofanya Tenga kwa miaka yake minane akiwa kiongozi mkuu wa soka la Tanzania.
Rais wa Marekani, hayati Abraham Lincoln
alipata kusema: “Usipoona madogo aliyofanya kiongozi aliyekutangulia,
basi huwezi kuwa kiongozi bora wala mwananchi mwenye nia ya dhati ya
maendeleo.”
Itoshe kusema kwamba Tenga kafanya yake na atakayekuja naye afanye
yake ili kusogeza mbele gurudumu la maendeleo ya soka Tanzania, kwani
uongozi ni kupokezena vijiti.
Inahitaji kitabu kumchambua Tenga ambaye hadi sasa ni mmoja wa
wachezaji wa kipekee wa Tanzania walioshiriki kwa mara ya mwisho
michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, wakiiwakilisha Tanzania miaka 33
iliyopita nchini Nigeria.
Mapema mwanzoni mwa mwaka huu, Tenga alitangaza kutogombea tena urais
wa TFF na kuwaachia wengine, akisema sababu kuu ni kuwa muumini wa
vipindi au awamu za kiongozi.
Tenga ni mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)
na pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Kandanda Afrika
(CAF). Natambua busara za Tenga katika uamuzi huo, japo alichelewa
kuuweka wazi.
Ukimya wake uliwatia hofu baadhi ya wakereketwa wa soka Tanzania
waliokuwa wakimaliza lami na anga kwa safari zisizoisha mikoani.
Walifunga safari hizo kwa sababu ndiko kulikuwa kukifanyika uchaguzi
mbalimbali wa wajumbe wa mkutanao mkuu wa TFF ambao ndio wapigaji kura
kwenye uchaguzi ujao.
Lakini kwa wale wa karibu, walitambua nia ya Tenga tangu mapema na wao kuanza kujiandalia mazingira ya kumrithi.
Yote kwa yote, baada ya aliyoyafanya Tenga na miaka yake minane
aliyoitumikia nchi yake katika soka, swali linakujala; ni kweli
anaondoka Tanzania kutaka kwenda kutumikia Afrika?
Je, ni kweli Afrika sasa inamhitaji Tenga? Je, anao ubavu wa kweli wa
kupambana na bosi wake (rafiki yake)? Je, amejiandaaje na hili katika
kuepuka yaliyomkuta mwafulani huko Mashariki ya Kati?
Huu ni mjadala mpana sana, ambao majibu yake sina moja kwa moja, ila wakati ukifika tutajuzwa.
Natambua kuna tetesi, kama si sintofahamu, ya kwamba Tenga amepanga kupambana na Rais wa CAF, Issa Hayatou.
Rais huyu wa sasa wa CAF ameliongoza shirikisho hilo la soka barani
Afrika kwa zaidi ya miaka 28. Sidhani kama itakuwa kazi rahisi, lakini
naamini kuna umuhimu wa kujipanga.
Tenga hajaweka wazi nia yake hiyo, japo ukweli ni kwamba anasikilizia
upepo, wanajisemea watoto wa mjini, ili afanye uamuzi kamili.
Japo haijathibitika, Tenga ni mmoja kati ya watu wawili wanaotajwa
sana katika kurithi mikoba ya Mcameroon Hayatou anayeonekana kama kisiki
kwenye shirikisho hilo.
Tetesi za Tenga kutaka kuvaa viatu vya Hayatou zilianza siku nyingi,
japo zilizidi kupewa uzito kwenye Mkutano Mkuu wa CAF uliopita.
Katika mkutano huo uliofanyika visiwa vya Shelisheli, lilipitishwa
azimio linalodaiwa liliandaliwa na Hayatou ili kumhakikishia ‘ulaji’
kwenye uchaguzi ujao.
Azimio lenyewe lilifikishwa na la mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji ya CAF, Mohamed Raouraoua
wa Algeria, akitaka mabadiliko kwenye katiba ya CAF, kwamba anayegombea
urais wa CAF lazima awe mjumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho
hilo.
Hayatou anasemwa kuitengeneza ‘fitna’ hiyo, ambapo wajumbe, akiwamo
Tenga, walitakiwa kupiga kura za wazi kukubali au kukataa kubadilisha
kipengele hicho. Ukisema ‘ndio’ unamaanisha mgombra urais lazima awe
mjumbe wa kamati ya utendaji ya CAF.
Kwa ujasiri wa hali ya juu, Tenga moja kwa moja bila kutafuna maneno
wala kuona aibu, mbele ya vigogo wote wa CAF alikwenda kupiga kura ya
‘hapana’, kulikataa azimio.
Yaani Tenga alipingana na mapendekezo ya azimio la ‘mtu wa Hayatou’
au Hayatou mwenyewe la kurekebisha sheria hiyo inayowafunga watu wengine
kutogombea nafasi hiyo kama si wajumbe wa kamati ya utendaji.
Hapa ndipo wengi waliona kuwa Tenga ana nia ya dhati ya kushindana na
gwiji wa zamani wa mbio, Hayatou. Tenga alikuja kusema mara kadhaa,
baada ya hapo, kwamba alifanya anachoamini ni sahihi.
Azimio lilipita, kwa sababu kati ya wajumbe 13 wa kamati ya utendaji
ya CAF, ni Tenga pekee aliyepiga kura ya kukakataa badiliko hilo.
Wapo wengine walioweka wazi nia ya kupambana na Hayatou kwenye
uchaguzi mkuu ujao wa CAF utakaofanyika kwenye mji wa maraha ulioko huko
kusini magharibi mwa nchi ya Moroko uitwao Marakeshi mapema mwezi Machi
mwaka huu.
Mmoja wao ni Rais wa Shirikisho la Kandanda Ivory Coast na mjumbe wa kamati ya utendaji ya FIFA, Jacques Bernard Anouma.
Binafsi simpi nafasi kubwa sana Anouma, kutokana na rekodi yake
inayoweza kumponza hivyo asiaminiwe na marais wa vyama vya nchi za
Afrika na wajumbe wa baraza kuu la CAF.
Huyu ni mmoja wa watu wanaotajwa kuchangia kwenye ufisadi wa serikali ya aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo ambaye sasa anakabiliwa na mashitaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, The Hague, lakini hatuwezi kujua.
Kitendo cha Tenga kupingana na viongozi wenzake kwenye kikao hicho
kinaelezwa kumjengea heshima kubwa miongoni mwa wajumbe wa mkutano mkuu
wa CAF.
Zipo taarifa za chini chini zinazosema amekuwa akiungwa mkono na marais wengi wa vyama vya soka barani Afrika.
Hata hivyo, kuna eneo ambalo Tenga anasemwa anakosa uungwaji mkono,
nalo ni magharibi mwa Afrika, ambako inasemekana ndiko kuna ngome ya
Hayatou.
Sababu ya ngome hiyo ya Hayatou kuimarika ni kurejea kwa washirika wake wa karibu, Slim Aloulou na Amadou Diakite.
Aloulou ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya CAF, wakati Diakite ni
Rais wa Shirikisho la Soka nchini Mali. Wote ni wajumbe wa kamati ya
utendaji ya CAF na washirika wakubwa wa Hayatou.
Wawili hao walikuwa kwenye vifungo vya miaka miwili vya FIFA, baada
ya kukutwa na hatia ya kushiriki vitendo vya rushwa na ufisadi.
Eneo walimokamatiwa ni kwenye harakati za kugombea uenyeji wa kombe
la dunia mwaka 2018 na 2022, na sasa tayari wametumikia adhabu zao.
Kurejea kwao kwenye harakati za soka barani Afrika kunaelezwa kuwa moja ya nguzo muhimu kwa Hayatou kurejea tena uongozini.
Tenga anakubalika Afrika Mashariki na Kati pamoja na kusini na baadhi
ya maeneo ya magharibi na kaskazini mwa bara hilo, lakini kuna mtihani
mwingine anaoweza kukutana nao.
Huo ni kupingwa na baadhi ya marais wa vyama vya soka kusini mwa
Afrika, akiwamo Kalusha Bwalya wa Zambia ambaye amekuwa akimtetea na
kumuunga mkono Hayatou bila kificho.
Yote haya bado ni sehemu ya maoni na mtazamo wangu juu ya huko
anakodaiwa kutaka kwenda Tenga, mhandisi kitaaluma ambaye soka ni kipaji
chake.
Inawezekana likawa ni jambo zuri kwa Watanzania, lakini ikawa ni
safari ambayo mwisho wake utakuwa ni ile kauli ya kujaribu si kushindwa.
Pamoja na kuwa bado hajaweka wazi nia yake hiyo, najiuliza tena kwa
mara ya pili; je, Baada ya TFF ni kweli Afrika inamhitaji Tenga? Wakati
ukuta.
No comments:
Post a Comment