JAMALI MALINZI
SLP 10000 DAR ES SALAAM
13/FEBRUARI/2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
YAH:KUENGULIWA KWANGU KUGOMBEA URAIS WA TFF 2013
Ndugu zangu, kupitia vyombo vyenu vya habari ninaomba
nieleze umma wa watanzania hususani wadau wa mpira wa miguu yafuatayo kuhusu
kuenguliwa kwangu.
Awali ya yote nieleze kusikitishwa kwangu na maamuzi
yaliyotolewa na kamati ya rufaa ya TFF ya kuniengua kugombea urai s wa
TFF.Sikubaliani na maamuzi yaha.
Katika kuniengua kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF imetoa
sababu mbili (nanukuu magazeti ya jana tarehe 12/02/2013 maana hadi leo
sijakabidhiwa barua ya kuenguliwa)
1.Kukosa uadilifu kwa kupinga
waraka uliotolewa na TFF wa kubadili katiba ya TFF mwezi Desemba 2012.
2.Kukosa uzoefu wa miaka mitano ya uongozi.
Ndugu zangu kiini cha maamuzi ya kamati ya rufaa dhidi yangu
ni pingamizi lililowekwa na mtu mmoja anayeitwa AGAPE FUE. Bwana Agape Fue
aliniwekea pingamizi katika kamati ya uchaguzi akidai mimi nilipinga waraka wa
kubadili katiba ya TFF na pia sina uzoefu uzoefu wa mika mitano ya uongozi wa
mpira. Kinyume na matakwa ya kamati ya uchaguzi kama yalivyotangazwa kuwa mtoa
pingamizi aje mwenyewe kutetea pingamizi lake , bwana Agape Fue hakutokea mbele
ya kamati ya bwana Lyato. Matokeo yake tarehe 31/01/2012 kamati ya uchaguzi ya
TFF ilitoa maamuzi ya kutupilia mbali pingamizi hilo.
Bwana Agape Fue hakuishia hapo kwa mara nyingine tarehe
06/02/2013 alikata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya uchaguzi akidai kamati ya
uchaguzi haikumtendea haki. Rufaa hii haikuwa na anwani wala namba ya simu ya
Bw Agape Fue ilisikilizwa tarehe 10/02/2013 na maamuzi ya kukata jina langu
yakatangazwa jioni ya tarehe 11/02/2013.
Mpaka leo najiuliza hivi huyu Bw Agape Fue ni mwanaume au ni
mwanamke? (hakueleza kama ni Bwana au Bibi Agape Fue). Agape Fue ni nani hasa?
Anaishi wapi? Je ni Mtanzania au sio Mtanzania maana kikanuni wasio watanzania
hawaruhusiwi kujihusisha na uchaguzi wa TFF (rejea kifungu cha 9 cha kanuni za
uchaguzi),pingamizi lake halikuambatana na udhibititisho wa uraia. Kwa nini
alichukua maamuzi haya? Sipata jibu. Iweje achukue maamuzi mazito ya kumkatia
mtu rufaa kisha uishie kusaini karatasi na kwaachia wengine wakusemee na usije
hata kushuhudia kinachoendelea kama kweli una maslahi na madai yako? Waandishi
wa habari mnisaidie kupata majibu.
Ndugu zangu, mtoa pingamizi alidai haikuwa sahihi kupinga
azimiao la kubadili katiba ya TFF kwa njia ya waraja . Naomba nisisitize mambo
matatu:
1. Wajumbe
wa mkutano mkuu wa TFF wanawakilisha matakwa ya vyama vilivyowatuma kwenda
kwenye mkutano mkuu wa TFF, na ndio ndio maana chama cha mpira cha mkoa wa
Kagera(KRFA) kiliitisha kikao cha kamati ya utendaji ili kamati iweze kutoa
mwongozo kwa wajumbe wake kuhusu nini kifanyike kuhusu waraka ulioletwa na TFF,
hivyo maamuzi ya yaliyotolewa ya kuukataa waraka huo yalikuwa ni maamuzi ya
chama cha mpira mkoa wa Kagerana wala haya kuwa maamuzi maamuzi ya Jamali
Malinzi, iweje Malinzi niadhibiwe kwa maamuzi haya, kwani nini usiadhibiwe mkoa
mzima na mikoa yote iliyopinga waraka? Hii ni haki kweli? Siamini kama kuna
mjumbe wa mkutano mkuu aliyekiuka maamuzi ya kamati yake ya utendaji.
2. Katika
mchakato wa kubadili katiba kwa njia ya waraka kilichokuwa kinagomba sio
maudhui (content) ya mabadiliko ya katiba bali utaratibu uliotumika kubadili
katiba. Swali la msingi tulilojiuliza ni wajumbe wa kamati ya utendaji KRFA ni
kwamba je kwa mujiibu wa katiba ya TFF kifungu 22 na kifungu 30 wapi katiba
inatamka kuwa inaweza kubadilishwa kwa njia ya waraka? Mpaka leo hilo jibu
hakuna , labda aliyeniwekea pingamizi atusaidie kupata jibu la swali hili.
Katiba ya TFF iko wazi kabisa inatamka kuwa katiba itabadilishwa kwa njia ya
mkutano mkuu tu( General assembly).
3. Ni
kweli FIFA iliagiza yafanyike mabadiliko ya katiba ya kuingiza kipengele cha
‘club licencing’ katika katiba , lakini je FIFA katika agizo hilo ilisema
katiba ya ya TFF ivunjwe ili kutimiza azma hiyo? Ikimbukwe kuwa mwaka 2004 FIFA
iliagiza TFF aiingize kwenye katiba kipengele cha katibu mkuu awe wa kuajriwa
badala ya kuchaguliwa, agizo lilitekelezwa kwa kupitishwa na mkutano mkuu wa
TFF, iweje leo utaratibu huu ukiukwe? Hata majuzi CAF walipotaka kubadili
katiba ili Rais wa CAF atokane na wajumbe wa kamati ya utendaji jambo hili
lilitekelezwa kwa kuitisha mkutano mkuu wa dharura uliofanyika Seychelles
majuzi. Katiba ndio msingi mkuu wa
uendeshaji wa TFF, nitaipigania siku
zote. Huu ndio utaratibu , si CAF si
FIFA si vyama vyama vya mpira vya nchi, hakuna anayebadili katiba kwa
njia ya waraka, kama kuna mwenye ushahidi aulete.
Kuenguliwa jina langu eti kwa kuwa
nilipinga waraka wa kubadili katiba sio uamuzi sahihi.
Kuhusu uzoefu wa miaka mitano
katika uongozi:
Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi wa
TFF mwaka 2008 niligombea na jina langu lilikatwa na kamati ya uchaguzi ya
TFF. Nilikata rufaa katika kamati ya
rufaa ya TFF na kushinda . Hukumu hii ni halali hadi leo . Iweje leo miaka
minne baadaye kamati hiyo hiyo ya rufaa ( kubadili kubadili majina ya wajumbe
sio kubadili taasisi) inione sina uzoefu? Si hilo tu, hata katika kujaza fomu
namba moja ya kugombea niliambatanisha vielelezo vyote vya uzoefu wangu ikiwa
ni pamoja na kudhibitisha kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita
nimekuwa :
-Mjumbe wa Baraza la michezo mkoa
wa Dar es Salaam.
-Mwenyekiti wa kamati ya
mashindano chama cha mpira mkoa wa Pwani COREFA.
-Mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa wa
Kagera.
-Mwenyekiti wa chama cha mpira
mkoa wa Kagera.
Hii ni pamoja na kuongoza Yanga
2002 -2005
Hivi katika nafasi hizi za uongozi
ipi ni ya kuongoza ‘Bonanza’? Nimedhalilishwa sana.
HITIMISHO.
Vyombo vya habari kupitia nakala,
tahariri na maoni ya wasikilizaji /wasomaji/watazamaji vimesifia sana awamu
mbili za uongozi wa Bwana Tenga. Bwana Tenga amesifiwa kwa umahiri wake wa
kuleta utulivu katika sekta ya mpira wa miguu Tanzania. Amesifiwa kwa kujenga
taasisi imara ambayo mhimili wake mkuu ni sekretarieti makini na kamati
mbaloimbali zilizo imara. Let him rise to the occasion, muda wa kuonyesha
uongozi imara ni huu, historia itamhukumu kwa jinsi gani atasimamia suala hili
, haki sio lazima itendekea lakini pia inatakiwa ionekane inatendekea.
Kamati ya utendaji ya TFF inayo
mamlaka ya kubatilisha maamuzi haya kwa maslahi ya mpira wa Tanzania.
Ninamshauri Rais wa TFF aitishe kikao cha dharura cha kamati ya utendaji ili
kijadili hali hii na kunirudishia haki yangu ya kugombea urais wa TFF.
Nihitimishe kwa kuwaomba wadau wa
mpira wa miguu Tanzania wawe watulivu wakati tukisubiri kupata ufumbuzi wa
suala hili
Mungu ibariki Afrika,
Mungu ibariki Tanzania.
Ahsanteni sana.
Jamali Emil Malinzi
Dar es Salaam
13/02/2013
No comments:
Post a Comment