VIONGOZI
wa mataifa mbalimbali duniani, kila mara wanakutana katika vikao vya
kimataifa kusaka amani, bila amani hakuna kitu chochote kinachoweza
kufanya nchi isonge mbele.
Utasongaje
mbele wakati kila saa ni migogoro na vita? Lakini Watanzania tumejaliwa
kwa kiasi kikubwa kuwa na amani, ambayo kwa sasa kuna baadhi ya watu
wanataka kuichezea. Ni kama vile wamechoka nayo.
Lakini
wakati kukiwa na migogoro mingine ambayo haina tija, kuna kitu ambacho
kimeanzishwa ili kuwakumbusha Watanzania kuhusu misingi halisi
tuliyowekewa na waasisi wa Taifa hili.
Hiki
si kingine isipokuwa ni mbio za Uhuru Marathon, ambazo zitafanyika
mwishoni mwa mwaka huu huku Rais Jakaya Kikwete kwa kuona umuhimu wake
naye ameamua kushiriki kama kinara na jemedari wa Taifa hili ambapo mara
kwa mara amekuwa akiwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa kuenzi amani
iliyopo..
Akithibitisha
hilo, Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck, anasema lengo la
mbio hizo ni kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kukumbuka, kuzingatia na
kuuenzi urithi waliaochiwa na viongozi waliopigania uhuru wa nchi.
Anasema
urithi huo ambao utakuwa ukikumbukwa kila mwaka kupitia mbio hizo, ni
upendo, mshikamano, umoja na amani iliyopo. Melleck anasema mbio hizo
zitakuwa zikifanyika kila mwaka na zitaanza rasmi siku ya tarehe
08/12/2013 na zitatanguliwa na shamrashamra za kanda zote za Nchi yetu.
Hilo
lilithibitishwa pia na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dk. Fenella Mukangara , ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati zinazinduliwa
jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi
wa mbio hizo ulienda sambamba na kuzinduliwa rasmi kwa mtandao wa Uhuru
Marathon ambao utakuwa na habari za kila aina kuhusu mbio hizo na
washirika wake.
Dk.
Mukangara alipongeza wazo la kuanzishwa mbio hizo ambazo zitakuwa
zikifanyika kila mwaka, lengo likiwa ni kudumisha umoja, amani na upendo
miongoni mwa Watanzania na kuuenzi uhuru wetu.
Waziri
alikiri, kwa sasa kuna mbio nyingi za marathon hapa nchini, lakini
hakuna ambaye alikuja na wazo zuri la kuanzisha mbio kama hizo za
kuuenzi uhuru wetu na kudumisha amani nchini.
“Nawapongeza
waandaaji wa mbio hizi ambao ni vijana wa Kitanzania waliokuja na wazo
hili zuri la kuanzisha mbio za uhuru. Tunazo mbio nyingi sana hapa
nyumbani, lakini hatukuwa tumewaza kuanzisha mbio zinazolenga kuuenzi
uhuru wetu na kudumisha amani yetu.
“…
Kwa niaba ya Serikali, napenda kusema wazi kuwa tumefurahishwa sana na
wazo hili la kuanzisha mbio hizi za Uhuru na nichukue fursa hii kuwaomba
wadau na wapenda maendeleo ya michezo kuungana na taasisi hii
kufanikisha mpango huu ili uweze kuwa na mafanikio.
“Serikali
bado itaendelea kuweka miongozo na mazingira rafiki ya kushirikiana na
wadau wenye nia nzuri ya kuendeleza michezo nchini. Nina hakika
waheshimiwa mawaziri, wabunge, viongozi mbalimbali wa Serikali,
mashirika binafsi na viongozi wa dini wote watajitokeza kushiriki mbio
hizi,” alisema.
Hapa
ndipo tunapoweza kusema kwamba, fikiria mbio zozote kubwa duniani kama
vile London Marathon nchini Uingereza, Paris Marathon, Ufaransa au zile
zingine zenye kupendwa na wengi zaidi duniani za Berlin Marathon
zinazofanyika Ujerumani kila mwaka, lakini Uhuru Marathon ni zaidi ya
mbio.
Kwani
mashindano yote haya ni ya kutukuka, kutokana na kushirikisha
wanariadha wenye majina makubwa duniani, huku kukiwa na ushindani mkubwa
zaidi miongoni mwa washiriki.
Lakini kwa sasa Tanzania ina cha kujivunia zaidi kwa ujio wa mashindano ya mbio Uhuru Marathon.
Upekee
wa shindano hilo la Uhuru Marathon ni kutokana na aina ya washiriki
wake, pamoja na kupewa tafu kubwa na waandaaji wa mashindano ya Berlin
Marathon, ambao wanataka kuiona Tanzania inatangazwa zaidi.
Hivyo,
shindano la Uhuru Marathon, lina nafasi kubwa ya kuwabeba Watanzania
kwa kutangazika zaidi, hasa ukichukulia uzoefu mkubwa walionao waandaaji
wa Berlin Marathon ikiwa pamoja na kuchangia kudumisha amani na upendo
nchini.
Mratibu
wa mbio hizo, Innocent melleck anasema, ana imani mbio hizo zitajizolea
umaarufu mkubwa, kutokana na jinsi zitakavyoteka hisia za watu
mbalimbali, wakiwemo wanamichezo.
Katika
mbio hizo, zitakazowashirikisha watu wa kada mbalimbali, zitakuwepo pia
mbio za kilomita 3, kilomita 5, Half Marathon kilomita 21 pamoja na
Full Marathon yenyewe kilomita 42.
Mratibu
huyo anasema mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi
wa kada mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia
zitakuwa za kuchangia kwa ajili ya watu wa mahitaji ya aina mbalimbali.
“Hapa
tunachotaka kufanya katika mbio za kilomita 3 ni kuwaomba kama vile
viongozi maarufu wa dini mbalimbali pamoja na viongozi wetu ili
kushiriki, kwa kudumisha amani na upendo.
“Pia
tutahakikisha kama mbio za kilomita 5, zinakuwa kwa ajili ya kuchangia
watu wenye mahitaji mbalimbali na tayari tuna uhakika mkubwa wa
wanariadha maarufu zaidi duniani kushiriki,” anasema.
Mratibu
huyo anafafanua kuwa wamejipanga mno katika hilo ili kuhakikisha
wanafanya mambo makubwa zaidi na ambayo yataleta tija kwa taifa.
Wakati
Uhuru Marathon ikitambulishwa bungeni, kiongozi aliyeonekana
kufurahishwa zaidi na hilo ni Spika Anne Makinda, ambaye hakuishia
kulimwagia sifa tu, bali alitaka hata viongozi wahakikishe
wanalifanikisha.
“Ni
wazo zuri hasa katika kipindi hiki ambacho tunapigania amani na
mshikamano miongoni mwetu, tunatakiwa kuenzi mashindano kama haya ili
kutufanya tuwe wamoja zaidi,” alisema Spika Makinda.
Msaada wa Berlin Marathon
Melleck
anasema, wamefanya mazungumzo na waandaaji wa mashindano ya Berlin
Marathon, kwani hilo ni moja kati ya mashindano makubwa zaidi duniani,
likiwa linashirikisha washiriki mbalimbali walio maarufu zaidi.
Shindano
la Berlin Marathon au maarufu zaidi kwa jina la BMW Berlin Marathon
kutokana na kudhaminiwa na kampuni ya BMW ni maarufu zaidi ndani ya
Ujerumani na duniani kwa ujumla.
Shindano
hilo la Full Marathon la kiilomita 42.195 ambalo linawashirikisha
wanariadha wa kulipwa na wale wa ridhaa, lilianza kwa mara ya kwanza
mwaka 1974 na linafanyika kila wiki ya mwisho wa Septemba kila mwaka.
Shindano
hili kwa umaarufu wake, mwaka 2008 lilishirikisha wanariadha takriban
40,827 kutoka mataifa 107, huku waliomaliza mbio wakiwa 35,913 na lina
zawadi mbalimbali za kuvutia.
Uhuru Marathon je?
Melleck
anasema, ushirikiano wa Berlin Marathon una maana kubwa, kwani
itasaidia kuitangaza zaidi Tanzania na kuifanya dunia itambue umuhimu wa
amani, upendo, umoja na mshikamano miongoni mwetu.
“Wanariadha
wengi watashiriki katika mbio hizi, wengi wakiwa maarufu zaidi duniani,
pamoja na viongozi wa kada mbalimbali na hivyo kutimiza lengo
tulilojiwekea.”
Mratibu
huyo anasema, kuna kila haja kwa Watanzania, kuyathamini mashindano
hayo, kwani yana lengo la kuwafanya wawe wamoja zaidi, hasa katika
kipindi hiki kigumu ambacho kuna majaribu ya kila aina.
“Waasisi
wetu wa taifa na wale waliopigania uhuru, walikuwa na malengo mengi na
tunatakiwa kuyadumisha hayo, hilo ndilo Uhuru Marathon
inalotakapigania,” anasema.
Kwa
Watanzania itakuwa faraja zaidi, hasa ukichukulia jinsi taifa
linavyoweza kufaidika kwa kuzalisha pia wanariadha wa aina mbalimbali.
Hivyo Uhuru Marathon ni zaidi yambio, kwani inatukumbusha tulipotoka, tulipo na tunapokwenda!
No comments:
Post a Comment