Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limepitisha sheria ya ‘ovyo’
ambayo mchezaji akifanya kosa katika mechi za kimataifa za klabu, kosa
lake litaiathiri pia timu ya taifa lake kwani hataruhusiwa kucheza hadi
amalize kutumikia adhabu husika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema
kuwa CAF wameagiza wanachama wake kuzingatia sheria hiyo ambayo itahusu
makosa ya kinidhamu na makosa mengine yanayofanywa na mchezaji katika
mechi za klabu za kimataifa.
“CAF wameagiza hivyo na hatuna namna kwa sababu sisi ni wanachama
wake. Mchezaji akionyeshwa kadi nyekundu au kadi mbili za njano na
kumlazimu akose mechi moja ama mbili, basi kama kuna mechi ya timu yake
ya taifa itakayofuata maana yake ataikosa kwa sababu ya kutumikia adhabu
hiyo,” alisema Osiah.
“Tunaomba wachezaji wawe na nidhamu ya hali ya juu katika mechi za
klabu zao kwani mambo sasa ni magumu. Makosa ya mchezaji ndani ya klabu
yataigharimu pia timu yake ya taifa,” alisema zaidi Osiah.
Katika siku za hivi karibuni, CAF wamekuwa wakiibuka na kanuni na
sheria ambazo nyingine zimekuwa hazilingani kabisa na zile za
mashirikisho mengine duniani.
Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka jana, CAF ilipitisha kipengele cha
mgombea wa urais wa shirikisho hilo kuwakiwa atoke miongoni mwa wajumbe
wa kamati yao ya utendaji, suala ambalo lilipitishwa kwa kura nyingi
licha ya baadhi ya wajumbe, akiwamo Rais wa TFF, Leodgar Tenga kupinga
vikali kifungu hicho.
No comments:
Post a Comment