KKansela Angela Merkel amefadhaishwa na kashfa ya kukwepa kodi
inayomkabili rais wa timu ya mpira wa miguu ya Bayern Munich, Uli
Hoeness, huku Hoennes akisema hatajiuzulu kupisha uchunguzi unaoendelea
dhidi yake.
Msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert, amesema kwamba watu wengi
nchini Ujerumani wamefadhaishwa na Hoennes, na hivyo ndivyo alivyo pia
Kansela Merkel.
Kwa mujibu wa Seibert, Kansela Merkel amefadhaishwa zaidi kutokana na
ukweli kwamba Hoeness amekuwa kielelezo chema kwa Ujerumani, kwani sio
tu kwamba anaongoza klabu bora kabisa ya mpira, bali pia amekuwa akiunga
mkono jithada kadhaa za maendeleo, ukiwemo mradi wa kuwajumuisha wageni
kwenye jamii ya Ujerumani.
Mwishoni mwa wiki, Hoeness alinukuliwa na gazeti la kila wiki la Focus
akisema kwamba aliripoti mwenyewe kwa mamlaka juu ya akaunti yake ya
fedha kwenye benki moja nchini Uswisi hapo mwezi Januari.
Waendesha mashitaka wamekiri kwamba wameanzisha uchunguzi huo kufuatia
ripoti iliyopelekwa kwao na Hoeness mwenyewe kupitia mshauri wake wa
masuala ya fedha .
Hoeness hatajiuzulu
Rais wa Bayern Munich, Uli Hoeness (kushoto) na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (wa pili kushoto).
Hata hivyo, Hoeness, mwenye umri wa miaka 61, amesema hana
mpango wowote wa kujiuzulu kutokana na tuhuma hizo za kukwepa kodi.
Badala yake, rais huyo wa Bayern Munich, ambaye pia ni mwenyekiti wa
bodi ya timu hiyo, ameliambia gazeti la Sport Bild Plus, atahudhuria
kweye mechi ya nusu fainali ya Champions League kati ya timu yake na
Barcelona hapo kesho.
Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Munich, Ken Heidenreich, amethibitisha
kuendelea kwa uchunguzi dhidi ya Höness, ingawa hakutaja kiwango cha
fedha kinachohusika wala muda ambao uchunguzi huo utachukua.
Mwenyewe Hoeness, ambaye pia ni mmiliki mwenza wa kiwanda cha kusindikia
nyama, amekataa kuingia undani wa suala hili, lakini ameahidi kutoa
ushirikiano wowote unaohitajika kwa waendesha mashitaka.
Ripoti hizo za kukwepa kodi ndizo zilizohanikiza kwenye vyombo vya
habari nchini Ujerumani na Hoeness amenukuliwa na gazeti la Münchener
Merkur, kwamba atajitetea kisheria dhidi ya vyombo vya habari
viinavyomtuhumu.
Höness, ambaye mwenyewe ni mchezaji wa zamani wa Ujerumani ya Magharibi,
amekuwa msemaji mkubwa kwenye soka ya Ujerumani, Bundesliga. Alikuwa
meneja wa kwanza kijana kabisa kwenye Bundesliga, baada ya kuchukua
nafasi hiyo akiwa na miaka 27 tu, kufuatia jeraha lililohitimisha
uchezaji wake uwanjani.
Baada ya zaidi ya miaka 30 akiwa kama meneja wa kibiashara wa Bayern
Munich, mwaka 2009 alimrithi Franz Beckenbauer kama rais wa timu hiyo.
Chini ya uongozi wake, klabu hiyo imekuwa na mafanikio zaidi kuliko
klabu zote za mpira nchini Ujerumnai na moja ya klabu tajiri kabisa
duniani.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman
No comments:
Post a Comment