HABARI mpenzi msomaji wangu. Leo imekuwa bahati kwani wiki hii
niliamua kutembelea Shule ya Msingi Mtakuja, iliyopo Kunduchi Mtongani,
Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kuiona shule hiyo niliyosoma
miaka kumi na tatu iliyopita, inaendeleaje.
Nilikwenda kutazama jinsi sera ya michezo mashuleni inavyofanya kazi,
ambapo nilikutana na mengi ambayo yanasikitisha, lakini wakati mwingine
inabidi ucheke - si kwa furaha, bali cheko la masikitiko ndani yake.
Jambo la kwanza niliingia kwenye darasa ambalo halikuwa na mwalimu,
ambalo lilikuwa lina makelele utafikiri sokoni Kariakoo. Kama ilivyo
ada, ratiba za vipindi hupachikwa nyuma ya mlango, somo la mchezo kwenye
ratiba lipo na kwa bahati kipindi kilichokuwa kinafuata ni cha michezo.
Nilitoka nje na kukaa kwenye bustani, kusubiri nione kama mwalimu
ataingia huku nikizungumza na wanafaunzi hasa mambo ya michezo, wengi
wao wakiwa hawajui kabisa kuhusu UMISHUMTA na UMISETA, ambayo ni michezo
maarufu ya kubuia vipaji shule za msingi na sekondari kwa Tanzania.
Lakini michezo hiyo imerudi mashuleni kinadharia na si kwa kivitendo.
Siasa imekuwa tatizo kubwa katika tasnia ya michezo mashuleni na
kwingineko, kutokana na ukweli kuwa, viongozi wengi wamekuwa wakiongoza
vyama au klabu na kisha kuziacha na kukimbilia siasa.
Hapa simsemi Katibu wangu wa zamani wa TFF, Fredrick Mwakarebela,
ambaye binafsi kwangu ni mwadilifu. Katika kukaa na wanafunzi wale
nilikuwa nataka kuelewa uwelewa wao wa michezo, siku hiyo kulikuwa na
darasa la nne, sita na saba, na kwa muda niliozungumza nao mpaka
namaliza, sikuona mwalimu yeyote wa somo hilo akiingia darasani,
nikahisi labda siku hiyo hakuwapo.
Wanafunzi wakaniambia somo la michezo huwa tunafanya mtihani tu,
sikushangaa sana kwani ndio mfumo ambao hata mimi ninayeandika makala
hii nilipitia. Lakini wakati huo sera ya michezo ilifutwa kwa kigezo
kuwa wanafunzi wanafeli sana mashuleni.
Kuna mwalimu ambaye sitamtaja jina, aliniambia serikali haijaleta
mwalimu wa michezo na hata mipira, ambayo mashuleni ipo ya wanafunzi
wenyewe ambao wanahusudu soka na huja shule na mipira waliyonunuliwa na
baba zao nyumbani.
Wanafunzi walio wengi, walionyesha uelewa kwa kufahamu kidogo katika
mpira wa miguu na kujua baadhi ya nafasi kiwanjani kama kipa, beki,
mshambuliaji, refa na mashabiki idadi ya wachezaji dimbani, basi.
Hii ni picha ambayo ukiitazama utaona dhahiri kuwa sera ya michezo
mashuleni imerudi kwa maandishi ya viongozi, lakini haijarudi rasmi
kivitendo na kwa nilichokigundua, inaonyesha dhahiri Tanzania bado tuna
safari ndefu kuelekea mafanikio, kwani yapo baadhi ya mambo muhimu
tunayafanya kwa siasa tena za uongo wa hali ya juu.
Hivi kweli serikali imerejesha michezo mashuleni, au ndio imetoa taa
ya kijani kwa wanafunzi kucheza bila mpangilio?
Jambo kuu ninalohisi
michezo imerudi kwa utashi wa kisiasa wanafunzi wengi ambao huanza
darasa la kwanza umri wao ni miaka saba umri sahihi kabisa wa
kumfundisha michezo.
Lakini wengi wa wanafunzi hawa ndio wa kwanza kucheza mpira kwa kutumia mashine za kompyuta ‘play station’.
Kubwa kati ya yote ambalo nasimamia mada yangu ya msingi ni kuwa,
kuonyesha kwamba michezo imejaa siasa, wakati wa uchaguzi viongozi wote
wa nchi hii waliwahi kuweka ligi za soka huku zikitumia majina ya
binafsi na kipindi hicho, huonyesha moyo thabiti wa kupenda na kundeleza
michezo ili tu waingie bungeni.
Wakifanikiwa, wanaanza kuulizia posho, hata kusahau walichotumwa na
wananchi, ukitazama hata bajeti ya michezo inatosha kulipia mishahara tu
ya Ofisa Utamaduni, na timu za taifa zinapokwenda nje kushiriki
michuano ya kimataifa, hupewa bendera na nasaha nyingi kana kwamba
walisaidia maandalizi.
Wachezaji wengi wa michezo mingi Tanzania, huwa wanacheza michezo hiyo
kwa juhudi binafsi na makocha hukutana nao wakati wakicheza kwenye
klabu kubwa.
Kwa mfumo huu ambao shule haina mwalimu wa michezo, mipira, viwanja na
kutokutilia maanani michezo, ni ndoto kabisa kuendeleza michezo. Tatizo
kubwa tumekuwa tukitaka kufanikisha mambo bila kufuata misingi ya
michezo, lakini tumekuwa hodari kusifia ufundi wa nchi za wenzetu kuwa
zinafuata maandalizi sahihi ya michezo.
Sisi siasa imechukua nafasi nyingi zaidi kila sekta, si michezo tu,
hata kwa mambo mengine. Nilipokuwa shule, mwalimu wangu wa Jiografia
alikuwa akifundisha na somo la Sanaa. Tulikuwa tukichora, huku
tunafundishwa muziki, japokuwa kinanda kilikuwa kinachorwa ubaoni,
lakini leo ukitaka muziki nenda Basata ukafundishwe kozi na King Makusa
na Juma Ubao.
Siasa imeharibu mifumo mingi ya uendelezaji soka, binafsi namsimfu
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika uongozi wake alijenga viwanja
vingi vya soka, ambavyo zama za sasa vinatia kichefuchefu hata kuviona.
Siasa hizo!
No comments:
Post a Comment