HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

22 April 2013

TENGA AGAWA MIPIRA 1,200 MIKOANI


 

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa mipira zaidi ya 1,200 yenye thamani ya dola 30,000 za Marekani kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na vituo 21 vilivyo hai vya kuendeleza vijana (academies).

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) lilimpa Rais Tenga fedha hizo ikiwa ni shukrani kwake kwa kushughulikia mgogoro wa uongozi wa mpira wa miguu nchini Kenya uliodumu kwa miaka miwili; ambapo nchi hiyo kutokana na mgogoro huo ilikuwa na vyama viwili (KFF na FKL).

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mipira hiyo kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Aprili 22 mwaka huu), Rais Tenga amesema amefanya hivyo kwa vile anaamini kuwa mipira ndiyo kitu muhimu katika kuinua mchezo huo mahali popote.

“Dhamira yangi si kushukuru kwa hafla hii, bali kutoa sababu kwa nini nimefanya hivi. Ninaamini kwa kuanzia mipira ndiyo muhimu, pili kwa kufanya hivi itaonekana kweli mipira imegawiwa,” amesema Rais Tenga.

Amesema amesema mpira wa miguu kwa Tanzania unahitaji sana watu wa kujitolea, na yeye amefanya hivyo kwa kujitolea kutokana na ukweli shughuli anazotumwa na FIFA ni za kujitolea.

Rais Tenga ambaye pia alitumwa na FIFA kutatua matatizo ya uongozi wa mpira wa miguu katika nchi za Uganda, Zambia na Sudan Kusini amesema anaamini anapata fursa hizo kutokana na kuwa kiongozi wa TFF, na kwa kuwakumbuka waliomchagua ndiyo maana hakusita kupeleka fedha hizo kwenye mipira.

Amesema moja ya ndoto zake wakati anaingia kuongoza TFF mwaka 2004 ameshindwa kutimiza ni kusaidia mipira, kwani uwezo wa kununua mipira kwa wanaocheza katika ngazi ya chini hasa watoto haupo.
“Hizi kelele zote za maendeleo ya mpira wa miguu ni kwa sababu shuleni hakuna vifaa. Nia yangu ilikuwa shule zote zipate mipira, lakini hiyo ni moja ya ndoto nilizoshindwa kutekeleza. Vipaji haziwezi kupatikana kama watoto hawachezi.

“Tunashukuru sana kwa Serikali kurejesha mpira shuleni. Hata nitakapoondoka madarakani nikipata nafasi nitaendelea kuomba mipira kwa ajili ya shule,” amesema Rais Tenga.

Vyama vya mikoa ambavyo jumla ni 32 (Tanzania Bara na Zanzibar) kila kimoja kimekabidhiwa mipira 25 (kumi saizi namba tano, 15 saizi namba nne kwa ajili ya vijana). Kwa academies ambazo ni 21 kila moja imepewa mipira 25 (minane saizi namba tano, na 15 saizi namba nne).

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Almasi Kasongo, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) Nassib Mabrouk na Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Riziki Majala.

Kwa upande wa shule alikuwa Kanali mstaafu Idd Kipingu ambaye ni mmiliki wa shule ya Lord Baden ya Bagamoyo mkoani Pwani.

COASTAL, AZAM KUCHEZA SIKU YA MUUNGANO
Timu za Coastal Union ya Tanga na Azam zitapambana Aprili 26 mwaka huu katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) itakayofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Awali mechi hiyo namba 168 ilikuwa ichezwe Aprili 27 mwaka huu, lakini imerudishwa nyuma kwa siku moja ili kuipa fursa Azam kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco.

Mechi hiyo itachezeshwa na Andrew Shamba kutoka mkoani Pwani akisaidiwa na Abdallah Mkomwa (Pwani), Vicent Mlabu (Morogoro) wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Mohamed Mkono wa Tanga. Charles Komba wa Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo ya raundi ya 24.

Baada ya mechi ya Tanga, Azam itarejea Dar es Salaam siku inayofuata tayari kwa safari ya kwenda Rabat itakayofanyika Aprili 28 mwaka huu. Mechi hiyo itachezwa wikiendi ya Mei 3, 4 au 5 mwaka huu.

Keshokutwa (Aprili 24 mwaka huu) kutakuwa na mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya African Lyon na JKT Ruvu itakayochezwa Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam.
Iwapo Azam itafanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho kutakuwa na marekebisho ya ratiba ya VPL. Hiyo ni kutokana na raundi inayofuata ya Kombe la Shrikisho kuchezwa wikiendi ya Mei 17, 18 na 19 mwaka huu ambapo bado haijajulikana Azam itaanzia wapi (nyumbani au ugenini) iwapo itavuka.

Mechi nyingine za VPL mwezi ni Aprili 25 (Ruvu Shooting vs Simba- Uwanja wa Taifa), na Aprili 28 (Simba vs Polisi Morogoro- Uwanja wa Taifa).

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers