WADAU
wa soka wa Zanzibar, wameibua mjadala juu ya hatua ya Chama cha Soka
Zanzibar kuitaka televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar, isiwaite
kuchambua masuala ya chama hicho kupitia kipindi cha ‘Sports Michezo’
bila wenyewe (ZFA) kuwepo.
Kipindi hicho maalumu huandaliwa na mwanahabari Farouk Karim na kurushwa kila siku ya Jumamosi mnamo saa 3:00 usiku.
Wakizungumza
na gazeti hili kwa nyakati tafauti, wadau hao wamedai kuwa, ZFA si
chama cha watu wa kundi fulani bali ni cha wananchi wote na kwamba wana
haki kukijadili bila masharti yoyote.
Kocha
wa mabingwa wa soka Zanzibar KMKM Ali Bushiri Mahmoud, ameeleza kuwa,
kama watu watakutana kuzungumzia masuala ya mpira wa miguu nchini, ni
lazima pia watakigusa chama hicho kwa kuwa ndicho kilichopewa dhamana,
hatua hiyo inaonesha woga wa chama hicho, na viongozi wake kutokuwa
tayari kukosolewa wala kushauriwa, pale wanapofanya mambo kinyume na
matarajio ya wananchi na wadau wa soka.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Wazee Sports Salum Bausi Nassor, amesema
ingawa hafurahishwi na uamuzi huo, yuko tayari kukaa pamoja na viongozi
wa chama hicho wakati wa kipindi cha ‘Sports Michezo’ ili kila upande
uoneshe changamoto zinazolikabili soka la Zanzibar.
“Mimi
ninafahamu kuwa mara nyingi viongozi wa ZFA huitwa katika kipindi
hicho, lakini wanakwepa wakitoa sababu mbalimbali, sasa kwani nini sisi
tusizungumzmie soka letu mpaka wao wawepo? alihoji Bausi.
Naye
Hussein Ali Ahmada, mmoja wa waasisi wa Akademi ya kuibua na kukuza
vipaji ya Oranje iliyoko Kikwajuni, alisema haoni sababu ya msingi
kulazimisha kuwepo kwa viongozi wa ZFA katika kipindi hicho, kwani
wanaweza kujadiliwa na baadae wakipenda waombe muda wa kujibu kama
wanayo majibu.
“Tatizo
ninaloliona, ni kwamba viongozi hao wanataka wapambwe kwa sifa nzuri
hata pale wanapofanya madudu yanayochangia kuporomosha soka la Zanzibar.
Hawataki maovu yao yaanikwe na wala hawataki kubadilika”, alieleza.
Muandaaji
wa kipindi hicho Farouk Karim, alisema analazimika kuheshimu uamuzi wa
ZBC, lakini akadai mara nyingi amekuwa akiwaita viongozi wa ZFA lakini
wanapiga danadana.
Aidha, alisema kimsingi, ZBC na ZFA zote ni mali za wananchi ambao
wameonesha kuvutiwa na kipindi hicho, ambacho huwa kinajadili mada
nzito na muhimu inayokuwepo kwa wakati maalumu kuhusiana na maendeleo ya
michezo.
Baada
ya baadhi ya wadau kudai kuwa Kaimu Rais wa ZFA Haji Ameir Haji
ameitaka ZBC iwazuie wafanyakazi wake kuichambua ZFA kupitia ‘Sports
Michezo’, Ameir amedai alichoomba ni kutaka wasijadiliwe bila wenyewe
kushiriki mjadala wowote unaowahusu.
Aidha
aliwashutumu wadau hao kuwa wanatumiwa kuibomoa ZFA, na kuongeza kwamba
Jumamosi wiki hii yuko tayari kuitwa pamoja nao katika kipindi hicho
ili kuzungumzia mambo yahusuyo soka hapa nchini.
Alipoulizwa
Mkurugenzi wa ZBC Hassan Abdallah Mitawi, alikiri kuwa Haji Ameir
alikwenda ofisini kwake kupeleka madai ya kubomolewa ZFA na wadau,
lakini hawakuzuiwa kuijadili, bali ameagiza wakati wa kipindi hicho, nao
waitwe ili kupewa haki ya kujibu kama walivyoomba.
No comments:
Post a Comment