Taifa
Stars imeshindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya leo (Julai
13 mwaka huu) kufungwa bao 1-0 na Uganda (The Cranes) katika mechi ya
kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Wachezaji wa Ligi
za Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Denis
Iguma ndiye aliyefunga bao hilo pekee kwa Uganda dakika moja baada ya
mwamuzi Thierry Nkurunziza kutoka Burundi kupuliza filimbi kuanzisha
kipindi cha pili cha mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Akizungumzia
matokeo hayo, Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesema mpira wa miguu ni
mchezo wa kufunga mabao ambapo timu ilipata nafasi nzuri katika dakika
ya kwanza tu lakini ilishindwa kuibadili kuwa bao.
“Uganda
walitengeneza nafasi moja tu katika kipindi cha kwanza wakati sisi
tulikuwa nazo kadhaa. Kipindi cha pili tuliwapa nafasi wakafunga bao
lao. Lakini kwa kifupi kama wao wameweza kufunga hapa (Dar es Salaam),
hata sisi tunaweza kufunga Kampala,” amesema Kim akizungumzia nafasi ya
timu yake kusonga mbele.
Timu
hizo zitarudiana jijini Kampala kati ya Julai 26 na 27 mwaka huu ambapo
mshindi ndiye atakayepata tiketi ya kwenda kwenye fainali za tatu za
CHAN zitakazofanyika Afrika Kusini. Stars ilicheza fainali za kwanza za
CHAN zilizofanyika mwaka 2009 nchini Ivory Coast.
No comments:
Post a Comment