Bert Trautmann na soka la Tanzania, alituwekea msingi…..
WIKI hii ulimwengu wa soka
umempoteza mmoja wa wataalam wa soka waliobobea, Mjerumani Bert
Trautmann aliyefariki dunia Ijumaa ya Julai 19, 2013 jijini Valencia
nchini Hispania alikoamua kuweka makao yake baada ya kustaafu shughuli
za soka. Amefariki akiwa na umri wa miaka 89 akikaribia miaka 90 kwani
alizaliwa jijini Bremen, Ujerumani Oktoba 22, 1923. Msiba huu unatugusa
Watanzania kwa sababu mtaalam huyo alikuwepo nchini mwetu mwaka 1975
katika kutimiza mpango maalum wa FIFA wa kutuma wataalam wake kuinua
soka kwenye nchi zilizokuwa chini kisoka.
Alianzia kutekeleza mpango huo Burma (1972-1974), akawa kwetu (1975),
kisha akaenda Liberia (1978-1980) na kumalizia mpango huo Pakistan
(1980-1983). Inaelezwa kuwa kutokukaa sana hapa kwetu kulisababishwa na
ugunduzi wake kwamba kisoka hatukuwa chini kihiiivyo kabisa kwa hiyo
alishauri aende maeneo hasa yaliyokuwa hoi kabisa kisoka. Usishangae
kuona Liberia alikaa kwa muda zaidi ya hapa. Walikuwa chini yetu hao na
ukweli ni kwamba hata sasa hawatuwezi.
Bert Trautmann, ambaye jina lake halisi ni Bemhard Carl Trautmann,
alikuwa mchezaji maarufu wa Manchester City kati ya mwaka 1949 na 1964
akicheza mechi 508 katika nafasi ya ukipa aliyokuwa akichezea. Cha
kusisimu, akiwa hapa kwetu alitengeneza timu ya makipa hodari tupu,
Athumani Mambosasa na Omar Mahadhi wote kutoka Simba ambao kwa sasa ni
marehemu. Aidha, alimuibua kijana mdogo wa wakati huo, Juma Nassor
Pondamali na kumfanya kuwemo kwenye timu ya taifa kukamilisha orodha ya
makipa watatu hodari tupu-Mambosasa, Mahadhi na Pondamali. Hii
isitafsiriwe kwamba utaalam wake hapa ulikuwa zaidi kwa makipa, hapana,
Trautmann, kama mtaalam wa soka, alifundisha mbinu za mpira kwa nafasi
zote akitupia macho umuhimu wa vipaji vya vijana na kutoa elimu kwa
makocha wetu wa wakati huo hasa Joel Bendera aliyekuwa msaidizi wake na
wengine kama kina Mohammed Msomali. Joel bendera kwa sasa ni Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro.
Kwenye kuwaamini vijana, mbali ya Pondamali, aliwainua kina Mohammed
Salim wa Coastal Union ya Tanga, Omari Hussein, Aluu Ali na Hussein
Ngulungu wa Mseto ya Morogoro na vijana wengine waliochipuka tu mwaka
huo 1975 na mwaka mmoja kabla. Ni kocha huyo ndiye aliyeona kuwa
Mohammed Kajole wa Simba (marehemu) ndiye aliyestahili kuziba pengo la
beki ya kushoto lililoachwa wazi na Mohahammed Chuma wa Nyota ya Mtwara
aliyestaafu kuchezea timu ya taifa mwaka huo baada ya kuichezea
mfululizo tangu mwaka 1964. Kama tulivyoeleza majuzi, Kajole aliitwa
kujiunga na wenzake Zambia kwenye mashindano ya Challenge ya mwaka huo.
Tuna kila sababu za kumkumbuka kocha wetu Bert Trautmann kwa sababu
msingi wa soka aliouweka uliimarishwa vizuri na waliompokea jukumu la
kuifundisha timu yetu ya taifa kwani miaka minne baadaye, 1979,
tulifanikiwa kukata tiketi ya fainali ya mashindano ya mataifa (huru) ya
Afrika nchini Nigeria, tuliyoshiriki mwaka 1980.
Katika historia ya maendeleo ya soka yetu, Watanzania hatupaswi
kumsahau Trautmann kwani alichangia kwa kiasi kikubwa kutuinua kisoka.
Mungu amlaze pema peponi mtaalam wetu wa soka Bemhard Carl Trautmann,
maarufu kama Bert Trautmann.
No comments:
Post a Comment