HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

3 July 2013

OBAMA NA KIKWETE WAONYESHA UFUNDI WA SOKA NA MUZIKI


Rais wa Marekani,Barack Obama(wa pili kushoto),akipasiana mpira na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete wakati alipotembelea kituo cha kufua umeme cha Symbion,Ubungo jijini Dar es Salaam jana.Mpira huo maalum una uwezo wa kufua na kutunza umeme unaoweza kuendesha vifaa vidogo vidogo kama kuwasha taa,tochi na kuchaji simu.
Rais wa Marekani, Barack Obama jana alithibitisha kuwa ni mwanamichezo wakati alipoonyesha ufundi wake wa kuuchezea mpira kwa kichwa na pia kupasiana na mwenyeji wake, Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete.

Tukio hilo lilitokea wakati Rais Obama alipotembelea mitambo ya kufua umeme ya Symbion, iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam katika siku yake ya mwisho ya ziara yake barani Afrika.

Mpira huo aliouchezea Rais Obama na Rais Kikwete ulikuwa ni wa teknolojia mpya wenye uwezo wa kufua na kutunza umeme unaoweza kuendesha vifaa vidogo vidogo kama kuwasha taa, tochi na kuchaji simu.

Rais Obama anafahamika kwa kupenda michezo mbalimbali ambapo hushiriki michezo kama kikapu na baseball.

Katika kuonyesha upenzi wake kwa mchezo wa kikapu, nyota wa Ligi Kuu ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA), Mtanzania Hasheem Thabeet katika hotuba yake fupi aliyoitoa wakati akizungumza na waandishi wa habari, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Obama alimtaja Thabeet kwa namna iliyoonyesha wazi kuwa anamfahamu vyema mchezaji huyo nyota wa timu ya Oklahoma City Thunder; huku akitania mwishoni mwa hotuba yake kwa kusema kuwa atamzungumzia siku nyingine.

Mtanzania Hasheem mwenye urefu wa mita 2.21, amejitwalia umaarufu mkubwa Marekani kutokana na uwezo wake uwanjani na pia kwa sababu hivi sasa ndiye mchezaji mrefu kuliko wote wanaocheza NBA.

Hasheeem alikwenda Marekani mwaka 2006 na kuanza kucheza NBA mwaka 2009 baada ya kusajiliwa na timu ya Memphis Grizzlies, hivyo kuandika rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kuwahi kucheza katika ligi hiyo yenye hadhi ya juu zaidi kwa mchezo wa mpira kikapu duniani.

Awali, kabla ya kuchomekea kwa utani jina la Hasheem katika hotuba yake, Obama alizungumzia namna Marekani inavyoshirikiana na Tanzania na mataifa mengine ya Afrika katika kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa nia ya kusaidia harakati kuliendeleza bara hili.

Aidha, juzi wakati akitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam akitokea Afrika Kusini, Obama alionekana kuvutiwa sana na ngoma mbalimbali za utamaduni alizochezewa wakati akipokelewa, zikiwamo za Mganda, Lizombe na Sindimba.

Kwa namna isiyotarajiwa, naye alijitosa na kuanza kunengua ngoma ya Mganda inayochezwa na wenyeji wa mkoa wa Ruvuma, huku akiungwa mkono na mwenyeji wake, Rais Kikwete na hivyo kuibua shangwe kubwa kutoka kwa wananchi waliokuwa wakishuhudia tukio hilo.

Kabla ya kuanza kucheza Mganda, Obama alianza kwa kumwaga tabasamu kuonyesha kuwa amevutiwa na ngoma hiyo, akawapigia makofi wanenguaji na mwishowe akahitimisha hisia zake kwa kuanza kucheza.

Kabla ya Obama kutua juzi, Rais Kikwete naye alionekana kuguswa na burudani ya ngoma zilizokuwapo uwanjani ambapo alikuwa akicheza kwa mtindo kama wa 'kiduku' muda mfupi kabla ya kuwasili kwa mgeni wake.

Katika hatua nyingine, mmoja wa watu waliofurahia salamu kwa kushikana mkono na kiongozi huyo alikuwa ni rais wa zamani wa klabu ya Yanga, Abbas Tarimba.
Obama aliondoka jana kurejea Marekani, baada ya kuzuru mitambo ya kufua umeme ya Symbion.

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers