Watanzania watano wamefanya mtihani wa uwakala wa
wachezaji wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao ulifanyika
jana (Aprili 3 mwaka huu) duniani kote.
Watahiniwa katika mtihani huo ambao ulikuwa na
maswali kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) walikuwa
Godlisten Anderson, Jesse Koka, Lutfi Binkleb, Rwechungura Mutahaba na Silla
Yalonde.
SIMBA KUIVAA KAGERA SUGAR VPL
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa
wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 24 kesho (Aprili 5 mwaka huu) kwa mechi
mbili ambapo Kagera Sugar itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba.
Mechi nyingine itakuwa kati ya Mbeya City ambayo
itakuwa mgeni wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi
jijini Dar es Salaam. Ashanti United inayofundishwa na Abdallah Kibaden ipo
katika mkakati wa kukwepa kushuka daraja.
Keshokutwa (Aprili 6 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati
ya Coastal na Mgambo Shooting Stars (Mkwakwani, Tanga), Oljoro JKT na Tanzania
Prisons (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Rhino Rangers na Mtibwa Sugar (Ali
Hassan Mwinyi, Tabora) na Yanga dhidi ya JKT Ruvu (Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam).
Raundi hiyo itakamilika Aprili 9 mwaka huu kwa mechi
kati ya Ruvu Shooting na Azam itakayochezwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani
Pwani.
NI MWADUI AU STAND UNITED VPL MSIMU UJAO
Ni ipi kati ya timu za Mwadui na Stand United, zote za
Shinyanga itakayocheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao itajulikana kesho
(Aprili 5 mwaka huu) baada ya kundi C kuhitimisha mechi za Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) msimu huu.
Mwadui yenye pointi 28 ndiyo inayoongoza, na itacheza
na Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Nayo Stand United yenye
pointi 26 itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Kambarage mjini
Shinyanga.
Mechi nyingine zitakuwa kati ya Pamba na Kanembwa JKT
itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Polisi Mara na Polisi
Tabora zitakwaruzana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Timu ambazo tayari zimepanda daraja kutoka FDL kucheza
VPL msimu ujao ni Ndanda SC kutoka kundi A na Polisi Morogoro ya kundi B.
21 ZA KUCHEZA RCL ZAJULIKANA
Timu 21 kati ya 27 zitakazocheza Ligi ya Mabingwa wa
Mikoa (RCL) kutafuta tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao
tayari zimejulikana.
Timu hizo ni Abajalo SC (Dar es Salaam), AFC (Arusha),
African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Geita Veterans (Geita), JKT
Mafinga (Iringa), JKT Rwamukoma (Mara), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United
(Pwani), Milambo SC (Tabora) na Mshikamano FC (Dar es Salaam).
Nyingine ni Mvuvumwa FC (Kigoma), Navy SC (Dar es
Salaam), Njombe Mji (Njombe), Pachoto Shooting Stars (Mtwara), Panone FC
(Kilimanjaro), Singida United (Singida), Tanzanite (Manyara), Town Small Boys
(Ruvuma), Ujenzi FC (Rukwa) na Volcano (Morogoro).
No comments:
Post a Comment