Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana
leo (Septemba 7 mwaka huu) na kupitia masuala mbalimbali ikiwemo mgogoro wa
kimkataba kati ya klabu ya Yanga na mchezaji Emmanuel Okwi.
Mkataba
huo ulipitiwa na Kamati ikiwemo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na upande
wa Yanga, na kuridhika kuwa mkataba kati ya pande hizo umevunjika.
Ukiwa
ni mkataba wa pande mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba 8 kuhusu malipo ya
ada ya usajili.
Yanga
ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia Juni 27
mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi
ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu yoyote.
Mkataba
ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi), ambapo Kamati imebaini
kuwa uhusiano huo haupo, hivyo hakuna mazingira ya pande hizo mbili kuendelea kufanya
kazi pamoja.
Pamoja
na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa wajumbe katika kikao kwa
sababu za kimaslahi (conflict of interests), walifahamishwa kuwa kilichopo
mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi, na si usajili.
Pia
lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya Misri. Kamati
imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na kulitolea
taarifa katika kikao kijacho.
Hata
hivyo mjumbe huyo hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa maamuzi. Uamuzi wa
kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na suala la kupiga kura.
Kuhusu
pingamizi la Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati imebaini kuwa klabu hiyo imevunja
mkataba kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa kumlipa mchezaji huyo mshahara
wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba.
Klabu
ya Coastal Union iliwakilishwa na mmoja wa viongozi wake, wakati Banda
aliwakilishwa na mwanasheria wake.
Vilevile
Kamati imekubaliana na pingamizi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro
(MRFA) kuhusu wachezaji waliofanyiwa uhamisho kutoka katika mkoa wake bila
kulipiwa ada za usajili, hivyo klabu husika zinatakiwa kulipa ada hizo.
Pia
Kamati imeagiza klabu zote zilizosajili wachezaji bila kuwafanyia uhamisho,
kulipa ada za uhamisho kwa pande husika kabla ya kuanza ligi, vinginevyo leseni
zao zitazuiwa hadi watakapolipa.
Mashauri
mengine ya pingamizi yatasikilizwa baadaye kwa vile klabu husika hazikupata
fursa ya kufika mbele ya kamati.
Kamati
inasisitiza kwa wanachama wa TFF kuheshimu mikataba.
No comments:
Post a Comment