HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

2 November 2012

Bingwa wa tenis walemavu aifagilia Tanzania



Bingwa wa tenis kwa walemavu wa viungo, Stephane Houdet amesema Tanzania ina kila kitu wakati linapokuja suala la uendelezaji wa mchezo wa tenis, na kwamba kinachotakiwa ni kuhamasisha wachezaji ili wajihisi furaha kucheza mchezo huo.
 Mcheza tenis huyo wa kimataifa kutoka Ufaransa aliyetua nchini Jumatatu kwa hisani ya Kampuni ya Saruji ya Tanga alisema kwamba vijana wengi wadogo wanapenda kucheza mchezo huo na kwamba ni lazima watiwe moyo kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya maendeleo yao.
 Houdet alisema inatia moyo kuona kwamba chama cha tenis nchini nchini kinafanya kila linalowezekana kuendeleza mchezo huo kwa kutoa nafasi sawa kwa watu wote wakiwamo walemvau.
 Nyota huyo wa tenis aliyasema hayo jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Klabu ya Gymkhana wakati wa ziara yake ambapo baadaye alikutana na wachezaji wa kawaida na walemavu kwenye Shule ya Sekondari ya Jangwani na pia makocha wa mchezo huo jijini Dar es Salaam.
 Houdet, aliyepoteza mguu wake mmoja baada ya kupata ajali mbaya ya baiskeli, aliachana na machungu tukio hilo kupata furaha kwa kucheza tenis ambapo sasa ni anashikilia nafasi ya tatu katika viwango vya ubora wa tenis duniani kwa wachezaji wa baiskeli za walemavu.
Houdet ana miaka 41 na sasa ni baba wa watoto wane.
WAKATI HUO HUO 
Mkutano mkuu wa Chama cha Soka cha Wanawake (TWFA) mkoa wa Morogoro umewachagua viongozi wake watakaokaa madarakani kwa miaka minne ijayo, ambapo mchezaji wa siku nyingi wa timu ya taifa ya soka ya wanawake, Edna Lema amefanikiwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti.

Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye Shule ya Msingi Bungo na kusimamiwa na viongozi wa kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA), Edna alishinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 15 kati ya 17 zilizopigwa, dhidi ya mbili za mpinzani wake, Mariam Naheka, aliyekuwa mwenyekiti wa muda, na ambaye hata hivyo hakuhudhuria katika uchaguzi huo kutokana na udhuru.

Mkurugenzi wa timu ya Morogoro Young Sisters, maarufu kama “Mama Yanga”, Pili Uledi, alijizolea kura zote 17 za ndiyo, akiwa hana mpinzani katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti huku Magreth Shaku, aliyekuwa katibu wa muda wa TWFA mkoa wa Morogoro, na aliyesimama bila mpinzani kutetea nafasi hiyo, aliidhinishwa rasmi kuwa katibu mkuu wa chama hicho baada ya kupata kura 15, huku kura mbili zikimkataa na Jovice Mwakasungula akichaguliwa kuwa msaidizi wake kwa kupata kura 14 na tatu zikimkataa.

Mwandishi wa habari wa magazeti ya kampuni ya Guardian na kituo cha Televisheni cha ITV na Redio One, kutoka Morogoro, Idda Mushi, alichaguliwa kuwa mwakilishi wa mkutano mkuu wa taifa wa TWFA, akimshinda Martha Mliga kwa kupata kura 9 dhidi ya 7 za mpinzani wake na kura moja kuharibika.

Hata hivyo kutokana na mwamko mdogo wa kisoka kwa wanawake, hasa katika kuwania nafasi za uongozi, nafasi za mweka hazina na wajumbe watatu wa kamati ya utendaji zilikosa wagombea na hivyo kamati iliyochaguliwa ikapewa rungu la kuziba nafasi hizo baada ya kuingia madarakani.

Akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu, Edna aliahidi kushirikiana na viongozi wengine kuhakikisha kuwa soka la wanawake linazidi kushika kasi mkoani Morogoro, ambako kuna vipaji vingi ambavyo vimekosa fursa ya kuibuliwa.

Katibu wa MRFA, Hamis Semka, aliwaasa viongozi wa TWFA mkoa wa Morogoro kutosita kuwafuata kwa ushauri wa masuala mbalimbali ya kiuongozi na kisoka ili kuhakikisha kwamba soka la wanawake linapanda chati Morogoro.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers