HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

21 January 2013

Louis Sendeu AIDAI YANGA (Sh. milioni 79.9)

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiwqMkCcmKCOCe8FLYB6BquO5_xu8zSZb6PEayWicGiaiw2rfwPspFdb7LC1apK24Os3qSFVVqdCzf28RjzrXmgbSN6jMeiuB7qScwg0yLxcfqcxxZ5uynRrIkaRBzq7Rt0OZ4LsVEPHAWk/s1600/sendeu.JPG


 Tuhuma za ufujaji wa fedha zitokanazo na jengo la kibiashara la Yanga lililopo katika Mtaa wa Mafia, Kariakoo jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa mambo yaliyozua mjadala mkubwa wakati wa mkutano mkuu wa mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwenye ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi jijini Dar es Salaam .

Baadhi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo walitaka maelezo ya kutosha kutoka kwa viongozi kuhusiana na jengo lao hilo, hasa mahala zinakokwenda fedha za kodi ya pango zinazokadiriwa kuwa ni mamilioni ya fedha.


Suala la jingo la Mafia, kuuzwa kwa kipa Shaaban Kado na ujenzi wa uwanja wa kisasa, ndizo ajenda zilizokuwa gumzo kwa kiasi kikubwa wakati wa mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama hai 1,444.


Iliwachukua takriban saa moja na nusu wajumbe wa mkutano huo kulijadili jengo la mtaa wa Mafia ambapo mwishowe, uongozi ulishindwa kutoa jibu la moja kwa moja na badala yake kuahidi kuunda kamati ya uchunguzi na kutoa maelezo ya kina ifikapo Februari 7 mwaka huu.


“Naona suala la Mafia ni kubwa, kila anayeinuka anazungumza kuhusu jingo la Mafia, wazee wetu Francis Kifukwe na Mama Fatma Karume wataunda kamati kufuatilia jengo letu maana wao ndiwo watunza mali za Yanga. Uhakiki utatolewa Febrauri 7,” alisema Clement Sanga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga.


Wanachama wengi waliopata nafasi ya kuchangia katika mkutano huo, walitaka kujua watu wanaokusanya mapato ya jengo hilo.


“Tunataka watu wanaojiona wajanja kwa kuhujumu mapato ya jengo la Mafia wajulikane na pia watambue kwamba jengo hilo ni mali ya Yanga. Si mali ya mtu ile,” alisema Hassan Chombe kutoka tawi la Dodoma.


UWANJA WA BIL. 32/-

Uongozi wa klabu hiyo ulitangaza kwa wanachama kuwa ujenzi wa uwanja wao wa kisasa utakaogharimu Sh. bilioni 32  utaanza rasmi Juni mwaka huu huku ukisimamiwa na kampuni ya Beijing Construction ya China, ambayo ndiyo iliyojenga Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Sanga alisema kuwa wameandaa mikakati mbalimbali itakayowawezesha kupata fedha za kufanikisha ujenzi huo ikiwamo ya kuwachangisha wanachama, kufanya harambee kwa wafanya biashara wakubwa na kuingia ubia na makampuni makubwa.


“Mpaka sasa hatujaamua uwanja huo utapewa jina gani. Kama kuna kampuni inataka tutumie jina lao, waje mara moja na kutupa pesa ili tujenge,” alisema Sanga huku akionesha michoro mbalimbali ya namna uwanja huo utakavyokuwa.


Akifafanua zaidi, Sanga alisema kuwa ujenzi wa uwanja huo utakamilika baada ya miaka miwili na wana mpango wa kulipanua eneo la makao makuu yao lilopo mitaa ya Twiga na Jangwani.


Kwa maelezo ya uongozi wa Yanga, uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 40,000.


SENDEU, MWESIGWA WATIMULIWA

Aidha, uongozi wa ‘Wanajangwani’ ulitoa orodha ya watu wanaoidai klabu hiyo hadi kufikia jana, ikionesha kuwa thamani ya madeni hayo inazidi Sh. milioni 200.

Miongoni mwa watu wanaoidai Yanga ni aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa (Sh. milioni 183.4) na aliyekuwa afisa habari wao, Louis Sendeu (Sh. milioni 79.9). Wote walisimaishwa kazi Septemba mwaka jana. Wadai wengine ni kampuni mbalimbali, zikiwamo za uwakili, hoteli na usafiri.


Mkutano huo uliamua kuwafuta uanachama Sendeu na Mwesigwa kwa kitendo chao cha kutokubaliana na klabu kuhusiana na fedha wanazodai ili kupata muafaka kwa njia za kiungwana, hasa kwa kuzingatia kuwa nao walikuwa ni Wanayanga.


KADO

Kuhusiana na Kado, gumzo lilikuwa ni kuuzwa kwa kipa huyo kwa Sh. milioni nne kwenda Coastal Union ya Tanga wakati Yanga walimtwaa kwa Sh. milioni 40 kutoka Mtibwa.

Hata hivyo, mwishowe wanachama waliusamehe uongozi kwa uamuzi huo ulioonekana kuwa ulifanywa kimakosa.

 

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers