Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, Issa Hayatou, amekubali kuwasilisha pendekezo mbele ya kamati ya utendaji ya CAF kuiondolea vikwazo ilivyoiwekea Togo.
Caf iliipiga marufuku Togo kushiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa miaka michuano miwili ijayo kwa madai ya serikali ya nchi hiyo kuingilia shughuli za soka wakati wa mashindano yaliyofanyika Angola ambapo Togo ilijitoa baada ya kushambuliwa.
Hatua hiyo mpya imetokana na upatanishi uliofanywa ambapo Shirikisho la Soka la Togo lilikiri kwamba halikufuata taratibu za CAF.
Kamati ya utendaji ya Caf inatarajiwa kukutana tarehe 15 Mei kwa uamuzi wa mwisho wa swala hilo.
Togo ilijitoa katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola baada ya basi lililokuwa limebeba timu ya taifa kushambuliwa na watu wawili kuuawa mwezi Januari mwaka huu.
Upatanishi
Upatanishi ulifanywa na rais wa FIFA,Sepp Blatter, baada ya pande zote kukubaliana kusitisha kesi iliyokuwa isikilizwe na mahakama ya upatanishi wa migogoro ya michezo (Court of Arbitration of Sport).
"Nina furaha kubwa kwamba tumeweza kupata ufumbuzi ambao umeridhisha pande zote," Bw Blatter alisema.
"Mafanikio ya leo ni kwa faida ya jamii nzima ya soka, hususan soka ya Afrika.
"Hii inaonyesha kuwa tunaweza kutatua migogoro ndani ya familia ya soka kwa faida ya wote wanaohusika na mchezo wetu, hasa kwa wachezaji".
Kwa hisani ya BBCswahili
No comments:
Post a Comment