Katibu mkuu wa shirikisho la kandanda Tanzania Osia Angetile |
Kumekuwepo na taarifa tofauti kuhusu
kuanza kwa Ligi Kuu ya Bara ambayo kwa mujibu wa kalenda ya Shughuli za
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), inatakiwa kuanza Septemba 01,
2012. Baada ya kikao cha pamoja baina ya TFF na viongozi wa klabu za Ligi Kuu
kilichofanyika Jumatatu ya Agosti 20, 2012 kwenye ofisi za TFF, TFF inapenda
kutoa ufafanuzi ufuatao:
1.
Baada ya kikao cha pamoja baina ya
TFF, Kamati ya Ligi na viongozi wa klabu zote za Ligi Kuu, ilionekana kuwa
kutokana na kutokamilika kwa mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya Ligi na mdhamini
wa sasa, yaani Vodacom, mwanzo wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa Septemba 15, 2012.
Hii inatokana na ukweli kwamba kukamilika kwa mazungumzo baina ya pande husika,
ndio kutatoa picha halisi ya Ligi Kuu ya msimu ujao.
2.
Mazungumzo baina ya TFF/Kamati ya
Ligi na Vodacom yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii kwa kuwa
yameshafikia hatua nzuri na hivyo mkataba unaweza kusainiwa wakati wowote baada
ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
3.
Kukamilika kwa mazungumzo hayo ni
muhimu kwa kuwa kutasaidia Ligi Kuu kuanza bila ya matatizo yoyote kwa klabu
zinazoshiriki, TFF na Kamati ya Ligi hasa kutokana na ukweli kuwa baadhi ya
mambo yatakayokubaliwa yatalazimika kuingizwa kwenye Kanuni za Ligi; yatasaidia
upatikanaji wa fedha kwa muda muafaka; upatikanaji wa vifaa kwa muda muafaka na
masuala mengine muhimu.
4.
Ratiba ya Ligi Kuu sasa inatarajiwa
kutangazwa mapema wiki ijayo pamoja na tarehe rasmi ya kuanza kwa Ligi Kuu
5.
Kutokana na kusogwezwa mbele kwa
tarehe ya kuanza kwa Ligi Kuu, mchezo wa Ngao ya Jamii baina ya mabingwa wa
Tanzania Bara na washindi wa pili, nao sasa utapangiwa tarehe nyingine ambayo
ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu. Kwa maana hiyo mchezo huo utachezwa
katika siku itakayotangazwa baadaye.
6.
Kuhusu chombo kitakachoongoza Ligi
Kuu, TFF ilitoa mapendekezo ya Kamati ya Utendaji kwa Kamati ya Ligi na baadaye
kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu kuhusu muundo wa chombo hicho kulingana na
mwongozo wa Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu
(FIFA) na Katiba ya TFF na suala hilo kwa sasa linajadiliwa na klabu za Ligi
Kuu kwa ajili ya hatua za mwisho.
Imetolewa Agosti 21, 2012 na
Angetile Osiah
Katibu Mkuu wa TFF
No comments:
Post a Comment