Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar Tenga amekataa barua ya kuomba kujiuzulu ya mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Ismail Aden Rage.
Rage ambaye pia ni Mwenyekiti wa
klabu ya Simba alimuandikia Rais Tenga barua ya kujiuzulu wadhifa huo kwa kile
alichosema ‘kamati hiyo kushindwa kwa makusudi kusimamia sheria na kanuni za
uendeshaji wa mpira Tanzania zinavyoeleza.’
Amekataa ombi hilo kwa maelezo kuwa
kama Rage amehisi kuwepo udhaifu wa kutosimamia sheria na kanuni kama
inavyotakiwa, ni vyema akaendelea kuwemo kwenye kamati hiyo ili kuisaidia
kusimamia sheria na kanuni hizo kama inavyotakiwa badala ya kujiuzulu.
“Kutokana na uzoefu na uwezo ambao
Rage anao katika uongozi wa mpira wa miguu, ni vyema akautumia kuisaidia kamati
kutekeleza wajibu wake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ili kusaidia
kusukuma mbele gurudumu za maendeleo ya mpira wa miguu,” amesema Rais Tenga.
Pia Rais Tenga amesisitiza kuwa ni
muhimu kwa mpira wa miguu kuongozwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo, rai
ambayo imetoa kwa kamati zote za TFF ili kuhakikisha kuwa mpira wa miguu
unaongozwa bila kuonea wala kupendelea upande wowote.
Rais Tenga amesisitiza kuwa kamati
hazina budi kuchukua hatua zinazostahili bila woga pale kanuni zinapotaka hatua
kuchukuliwa. Amezitaka kamati zisisite kwa namna yoyote ile kuchukua hatua kwa
vile kwa kufanya hivyo, uwezekano wa kutokea upendeleo au uonevu utapungua,
hivyo mpira wa miguu kuongozwa kwa sheria na haki.
No comments:
Post a Comment