Kamisheni
ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC) leo imelipiga jeki Shirikisho la
Ngumi za Ridhaa Nchini (BFT) katika mashindano yaliyomalizika katika
uwanja wa ndani wa Taifa leo tarehe 19/09/2012. Rais
wa TPBC bwana Onesmo Ngowi alimkabidhi Katibu Mkuu wa BFT bwana Makoye
Mashaga zawadi za washindi wa kwanza na wa pili katika mashindano ya
ngumi za ridhaa za taifa yaliyoshirikisha mabondia kutoka katika mikoa
zaidi ya 19 ya Tanzania bara.
Bwana
Ngowi alimweleza katibu Mkuu wa BFT kuwa TPBC inaungana na BFT katika
kuendeleza ngumi nchini wakijua wazi kuwa ni katika mashindano kama haya
Tanzania inawapata wawakilishi wake katika mashindano ya kimataifa.
Ushirikiano huu wa TPBC ulianza tangu wakati wa Katibu Mkuu wa zamani wa iliyokuwa TABA marehemu Narcis Tarimo.
Akimwelezea
zaidi msaada wa TPBC katika mashindano ya taifa, Rais wa TPBC bwana
Onesmo Ngowi alisema kuwa ni ngumi za ridhaa pekee ambazo zinaweza
kuleta mwelekeo wa maendeleo ya ngumi nchini.
Ngowi
alisema kuwa kama hakuna msingi mzuri wa ngumi za ridhaa ni wazi kuwa
hakutakuwa na ngumi nzuri za kulipwa kwani msingi wa ngumi unaanzia
kwenye ngumi za ridhaa.
Rais
huyo aliyekuwa bondia maarufu wakati wa ngumi za ridhaa na kulipwa
miaka ya 80 na 90 kiasi cha lupewa jina la “Piston Mover”(mwendo wa
piston ya gari) kwa ajili ya kasi ya mikono na miguu yake alisema kuwa
kuna umuhimu mkubwa wa kufundisha ufundi kwa mabondia ili waweze kucheza
ngumi za ufundi.
“Kuna tofauti kubwa sana kati ya ngumi za ridhaa na ngumi za kulipwa” aliendelea kusisitiza Rais huyo.
“Wakati
mabondia wa ridhaa wanapewa points wakati wanapopiga ngumi za ufundi za
kichwani, bondia wa ngumi za kulipwa anatakiwa aweze kumzidi mpinzania
wake kwa kila kitu” aliendelea kusisitiza Rais huyo.
Mabondia
wetu wa ridhaa wanatakiwa wafundishwe namna ya kupiga ngumi za ufundi
kichwani na ziwe nyingi ndipo wanaweza kushinda kwenye mashindano ya
kimataifa” alimalizia kusisitiza Ngowi.
Ushirikiano wa TPBC na BFT unaleta sura mpya kwenye tasnia ya ngumi nchini na inaonyesha mwanga mzuri mbele ta safari.
Mgeni
rasmi katika fainali za mashindano hayo alikuwa ni Katibu Mkuu wa BMT
bwana Henry Lihaya na alimshukuru Ngowi kwa msaada huo wa TPBC.
Aidha, Ngowi alikabidhi baadhi ya zawadi kwa washindi walioshinda katika fainali hizi za mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment