HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

11 October 2012

RVP AIPA FAIDA ARSENAL

By Israel Saria on October 11, 2012

*Wachezaji wana raha, wamejipanga upya

Robin Van Persie ameanza kusahaulika Arsenal, baada ya kuondoka majira ya kiangazi na kujiunga na Manchester United kwa dau la pauni milioni 24.
RVP aliondoka akiwa na hasira fulani na kukosa shukurani kwa waliomfikisha kileleni kisoka, akidai klabu imeshindwa kuweka sera madhubuti za kuleta .vikombe Emirates.
RVP amefunga jumla ya magoli 96 katika mechi 200 za ligi, ambapo msimu uliopita ndio alikuwa bora zaidi, akifunga magoli 30.
Ameshaondoka na sasa anachezea Mashetani Wekundu, na wadau wa Arsenal hawakuchelewa kupiga hesabu za faida za muda mfupi na mrefu za kumuuza Mdachi huyo.

Klabu Imepata Fedha Nyingi
Kitita cha pauni milioni 24 ilikuwa fedha nzuri kwa mchezaji ambaye umri wake unakwenda, aliyekuwa amebakisha msimu mmoja tu kwenye mkataba na aliyekwishatamka hataki kubaki klabuni.
Arsenal wangeweza kumbakisha kwa nguvu hadi msimu uishe, lakini hangecheza kama alivyokuwa, na mbaya zaidi angeondoka bila klabu kupata senti tano muda wake ukaisha.
Amani Inajengeka na Kudumu Klabuni
Itakumbukwa kwamba, Robin hakuwa akipenda mchezaji mwingine mwenye uwezo kumshinda, na hata lawama zake kwamba klabu hainunui wachezaji hazikuwa za dhati.
Robin anajulikana wazi kwamba hakufurahia jinsi wachezaji wa aina ya Aaron Ramsey walivyokuwa wakipanda chati klabuni hapo, hadi Ramsey akaja kuvunjwa mguu na mlinzi wa Stoke City, Ryan Shawcross; sasa Ramsey amerejea na anachanua.
Baada ya Ramsey kuumia, Wenger hakusajili mchezaji kwenye namba hiyo, lakini Robin aliendelea kujiona kama mfalme na kutotaka yeyote amfikie.
Hata alipoanza ngebe za kuondoka, inasemwa hakufurahishwa na kusajiliwa kwa Podolski, mtu ambaye ni wazi ni msaada kwa klabu na timu.
RVP angebaki, wachezaji wenzake ambao walishajua tabia yake wangejihisi vibaya, kwamba yupo klabuni tu kwa sababu anatakiwa wala hachezi kwa kujituma.
Hali hiyo ingeweza kusababisha akabaki anasononeka muda wote, na timu ingepata hasara. Ni bahati mbaya amekwenda kwa mahasimu wa Arsenal kisoka, lakini pesa tamu.
Kuondoka kwa RVP kunafungua mwanya kwa kizazi kipya cha washinda mechi kujitokeza na kujipanga, maana watu wa nje walikuwa wakidai kila wanaposhinda kwamba Arsenal wanabebwa na RVP.
Kukosekana kwake kunawafanya wengine wajitokeze kuchangia mabao na ushindi kwa timu.
Wapo akina Theo Walcott, Alex Oxlade-Chamberlain, Lukas Podolski, Gervinho na Santi Cazorla.
Olivier Giroud ameanza mambo yake, lakini pia kuna kinda la miaka 17, Serge Gnabry aliyejumuishwa kwenye kikosi cha ligi ya mabingwa Ulaya.
Kuondoka kwake kumetupilia mbali mtanziko uliokuwapo kwa wengi juu ya hatima yake, au kwamba Arsenal haingeweza kusimama bila yeye, akifuata msururu wa nyota walioondoka kabla yake, japo wengine waliaga kwa heshima bila dharau.
Ukweli leo hii ni kwamba Arsenal wanajiona hawatetereki hata aondoke nani. Hakuna tena kigugumizi kama kilichotanda wakati RVP akitikisa kibiriti. Sasa timu inajisuka vyema, imeanza vizuri ligi japokuwa bado kuna maeneo ya kurekebisha.



Donge nono lililopatikana kwa kumuuza RVP linaweza kuwekezwa kwa kununua wachezaji wanaohitajika, maana Kocha Arsene Wengere amekuwa akishutumiwa wakati mwingine kwamba hatumii fedha.
Lakini usajili wa Cazorla anayesemwa kuziba kabisa pengo la Cesc Fabregas na pia kununuliwa kwa Lukas Podolski na Giroud kunaonesha Wenger yu tayari kutumia fedha akiona inafaa.
Uuzaji wa RVP ulitokea baada ya watatu hao kusajiliwa, kwa hiyo bosi wa Washika Bunduki wa London ana fedha kibindoni kwa ajili ya kuimarisha kikosi Januari au hata kiangazi kijacho.
Pauni milioni 20 zinaweza kununua chipukizi kadhaa au mchezaji mmoja sampuli ya Cazorla.


Nahodha Mpya Ataleta Mambo Mapya
Kuondoka kwa Robin kunafungua mwanya kwa nahodha mpya kuleta utambulisho tofauti klabuni, badala ya uhafidhina ule ule wa zamani.
Licha ya tabia yake ya kutotaka wengine kumfikia kisoka, japo wanampita, kama nahodha yalihitajika mabadiliko.
Leo yupo Thomas Vermaelen, na kawaida ni kwamba manahodha wote huongoza kwa mifano yao wenyewe. RVP alifanya hivyo kwa kufunga mabao, Vermaelen anakuja kivingine na kujenga timu bora zaidi ya ushindi.
Wakati kama huu mwaka jana, Arsenal walikuwa wameshachakazwa vibaya sana, kwa wingi wa magoli na mechi walizoshindwa kwenye ligi, tofauti na sasa ambapo wamepoteza kwa tabu mechi moja dhidi ya Chelsea.
Ndiyo maana inasemwa RVP alikuwa akidaiwa kuwabeba Arsenal – katika njia sahihi au potofu. Sasa yupo kepteni mpya, mwenye moyo, dhamira, ni msemaji na ana uzoefu, pasipo upungufu wa kiwango cha teknolojia, basi sura mpya ya Arsenal inachanua.
Ni kweli kwamba kunyanyua kombe kwa timu iliyotoka patupu kwa miaka minane kingekuwa kipindi kizuri mno cha mpito kwa Mbelgiji huyu.
Hata hivyo, inatosha tu kwa sasa kwamba timu inakwenda vizuri, na yeye anazo sifa za kuwa kwenye nafasi hiyo, wenzake wakimuunga mkono.
 tanzaniasports


No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers