HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

10 November 2012

MDAU AJITOLEA KUANDIKA VITABU VYA MICHEZO



VUTA-NIKUVUTE: SIMBA VS YANGA – Hiki ni kitabu kinachohusu mechi karibu zote za Simba na Yanga kuanzia mwaka 1960 mpaka sasa. Kimejaa ripoti za mechi husika, mpira ulivyochezwa, kabla na baada ya mechi hali ilikuwaje (mnatambua kuhusu vimbwanga baina ya mashabiki wa timu hizi), pamoja na wafungaji wa mabao na vikosi vyao.

2. UBINGWA WA SOKA TANZANIA – Hiki kinahusu mashindano yanayoendelea sasa ya kutafuta klabu bingwa ya Tanzania. Zamani ilijulikana kama Ligi ya Taifa, sasa Ligi Kuu ya Vodacom. Ni dhahiri kwamba, wengi tumesahau ama hatujui kwamba mashindano hayo enzi hizo yalishirikisha pia mpaka shule za sekondari. Tena tusishangae kuona timu nyingi za majeshi hivi sasa, kwa sababu zilikuwepo pia. Mnatambua kwamba kulikuwa na Simba (Sunderland) na Yanga mikoani kama Tanga, Lindi, Morogoro na kadhalika? Kitabu hiki ndicho kimesheheni mambo yote ya soka, kikiwa na harahati za usajili, mechi zilizochezwa, takwimu zake, mapato na mambo mengine kama hayo.

3. TANZANIA NA MASHINDANO YA KIMATAIFA – Hiki kinazungumzia mechi za timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) katika mashindano mbalimbali ya kimataifa kuanzia Gossage (Challenge), All Africa Games, Olimpiki, Africa Cup of Nations, Kombe la Dunia na kadhalika.

4. KLABU ZETU KATIKA MASHINDANO YA AFRIKA – Sote tunatambua kwamba, klabu ya kwanza kushiriki mashindano ya Afrika ilikuwa Cosmopolitans mwaka 1968, ingawa ilishindwa kurudiana na timu ya Polisi ya Somalia kwa kugoma kupanda Land Rover 109. Lakini tangu hapo klabu zetu zimekuwa zikishiriki kila mwaka mashindano ya kimataifa, hasa ya Afrika. Hatujatwaa ubingwa, lakini tunatambua kwamba Simba ilifika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, imefika hatua ya makundi mara moja mwaka 2003, na Yanga nayo imefika robo fainali ya Kombe la Klabu Bingwa mara tatu – 1969, 1970 na 1998, na robo fainali ya Kombe la Washindi 1995. Malindi nayo imefika nusu fainali ya Kombe la CAF mwaka 1995 kabla ya kutolewa na Etoile du Sahel kwa mikwaju ya penalty 4-3. Haya yote, pamoja na matokeo ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati yatakuwemo pia.

5. YANGA: KLABU KONGWE ZAIDI AFRIKA MASHARIKI – Inazungumzia historia ya klabu ambayo leo hii inajulikana kama Yanga. Kitabu hiki kimeanza kueleza tangu harakati za timu za kizalendo zilizoanza mwaka 1926 na kuzaliwa kwa timu ya Jangwani Boys hadi magawanyiko na kuzaliwa Sunderland (Simba 1929) na baadaye kusajiliwa rasmi miaka ya 1930.

Wajumbe wenzangu,
Nimeamua kuleta barazani hili kwa sababu kumbukumbu hizi ni muhimu kwa taifa letu. Mimi ni kiumbe, na daima ‘Embe mbovu ina thamani ikiwa mtini, upepo ukivuma inadondoka na watu wataisahau’. Naweza dondoka leo au kesho, kumbukumbu hizi nazo zinaweza kupeperuka kwa upepo zikatoweka. Kuianza kazi upya ya utafiti kama nilivyoifanya itakuwa vigumu zaidi, maana naamini hata wale niliowahoji miaka 16 iliyopita wakati naanza utafiti wangu, baadhi yao wametangulia mbele za haki.
Nimejitahidi kuzunguka kwa wachapishaji mbalimbali, Uswahili ni mwingi. Kama mnavyojua, wengine tumejaaliwa mitaji ya mawazo, lakini hatuna uwezo wa kuendeleza hata pamoja na kukamilisha kazi husika. Anayejua maana ya utafiti anatambua ugumu uliopo, gharama ni kubwa, japo si za mara moja. Lakini gharama ni kubwa zaidi katika uchapaji, kwa sababu zinahitajika fedha za mara moja, ambazo mjumbe mwenzenu sina.
Kwa hiyo basi, yeyote mwenye kujua namna ninavyoweza kufanikiwa kuchapa vitabu hivi, au mwenye kuguswa kusaidia katika uchapaji, tafadhali ombi linakuja kwake kwa sababu ninaumia zaidi ninapoona kazi niliyoifanya, bila kutumwa na mtu, ikiendelea kubaki kabatini bila kuwasaidia Watanzania wenzangu.
Wadau wengi wa soka nimewaona, lakini (kama mnavyojua) kila mtu amekuwa na lugha yake, nyingine za kukatisha tamaa.

Tuwasiliane kwa yeyote mwenye kudhani anaweza kunisaidia.

Mjumbe mwenzenu,
Daniel Mbega,
Iringa – Tanzania
0655-220404/0784-939319/0767-939319

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers