Basi la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limekamatwa na madalali kwa amri ya mahakama kutokana na deni la sh milioni 140
ambalo tunadaiwa hadi litakapolipwa.
Amri hiyo imetokana na deni hilo la kampuni ya
Punchline ya Kenya iliyokuwa ikichapa tiketi za kuingilia uwanjani kuanzia
mwaka 2007. Hadi sasa tumeshalipa sh. milioni 70 katika deni hilo.
Jitihada zinafanyika ili kumaliza deni hilo. Pia
tunachunguza mwenendo mzima uliosababisha kuwepo deni hilo.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limezuia
mechi zake kuchezwa Guinea, Liberia na Sierra Leone kutokana na kuripotiwa
kuwepo kwa wagonjwa wengi wa Ebola katika nchi hizo.
Ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia kusambaa kwa virusi
vya ugonjwa huo kupitia mkusanyiko wa watu, CAF imevitaka vyama vya mpira wa
miguu vya nchi hizo kuchagua viwanja vingine huru kwa ajili ya timu zao
zinazoshiriki michuano yake kwa kipindi hiki hadi katikati ya mwezi ujao.
CAF itafanya tathmini nyingine kuhusiana na ugonjwa
huo kuanzia katikati ya Septemba ili kuona kama nchi hizo zinaweza kupokea timu
ngeni kwa ajili ya mechi mbalimbali za michuano yake, na baadaye kufanya uamuzi
wa kuruhusu au kuendelea kusimamisha.
Pia kutokana na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani
(WHO), CAF imesema kwa nchi zenye virusi vya Ebola ni muhimu kwa vyama vyake
vya mpira wa miguu kuufanyia vipimo vya afya msafara wa timu zao ili
kuhakikisha wenye virusi vya ugonjwa huo hawasafiri.
No comments:
Post a Comment