Kampuni
ya ASAR Entertaiment ikishirikiana na Ubalozi wa Switzerland na Kituo cha Ufaransa
cha Utamaduni, Alliance Française de Dar es Salaam, inakuletea maonyesho ya
Swahili Hiphop 2012 yatakayofanyika kwa siku nzima kwenye viwanja vya Alliance
Française siku ya alhamisi ya tarehe 22 ya mwezi huu.
Maonyesho
haya ni bure, kwa maana kwamba hakuna kiingilio, na bidhaa zitakazoonyeshwa ni
zile zinazotengenezwa na wasanii wa hiphop au vikundi mbalimbali vya vijana wa
Kitanzania, kama vile CDs (santuri), kanda mseto, majarida, posters, mavazi,
bidhaa mbalimbali za kitamaduni na kadhalika, lengo likiwa kuwapa nafasi ya
bure ya kuonyesha na kuuza kazi zao.
Pamoja
na mauzo hayo yatakayofanywa na wasanii arobaini wa hiphop, pia kutakuwa na
mafunzo ya nguzo tano za hiphop yatakayotolewa na wakufunzi waliobobea katika
nyanja hizo, ikiwemo vipindi vya u-dj, utunzi wa mashairi, utengenezaji wa ala
za muziki, upigaji machata (graffiti) na mabreka (breakdancing), ikifuatiwa na
burudani mbalimbali za u-MC zitakazotolewa na wasanii wakongwe na mahiri wa
hiphop.
Maonyesho
haya yataanza rasmi Saa Tatu asubuhi mpaka Saa Nne usiku, ikifuatiwa na siku
nzima (Ijumaa, 23 / 11 / 2012) ya Swahili Hiphop Summit 2012, mkutano
utakaofanyika katika ukumbi wa Alliance Française, tarehe 23 kuanzia saa mbili
asubuhi mpaka saa tisa alasiri.
Mkutano
huu utafunguliwa na balozi wa Switzerland nchini Tanzania, Mr. Olivier Chave na
utahudhuriwa na wageni waalikwa wapatao 200,
wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wa serikali, wakurugenzi wa
mashirika, wafanyabiashara, wadau mbalimbali wa muziki, wazazi, mashabiki na
wasanii wa muziki kwa ujumla, hususan wale wa hiphop.
Lengo
kuu la mkutano huu ni kujadili changamoto mbalimbali zinazoikumba tansia ya
muziki wa hiphop na njia za kutatua matatizo haya ambayo pia yanawakumba
wasanii wengine wasiofanya muziki wa hiphop.
Mijadala
mbalimbali itaendeshwa katika kufikia malengo ya kuwakomboa wanamuziki hawa,
ikiwemo suala zima la haki za wasanii, hati miliki, muziki kama biashara na
maisha, na hata tafsiri mbovu juu ya neno ‘hiphop’. Mkutano huu utakamilishwa
na kilingi cha wanamuziki wa hiphop, ama cypher kwa lugha ya kimombo,
itakayofanyika kwa kutumia midundo ya ngoma za kitamaduni.
Pia
jioni ya ijumaa hiyo, tarehe 23 / 11 kwanzia saa kumi na moja jioni, kutakuwa
na shoo kali ya uzinduzi wa santuri ya msanii mpya wa hiphop aendae kwa jina la
Randy ‘D Dawn kutoka kundi la Watanzah, atakayepanda jukwaani kwa kishindo akisindikizwa
na kundi lake hilo.
Shoo
hii ni bure kwa wote. Steji pia
itashambuliwa na wasanii wengine hatari katika hiphop akiwemo JCB na Mo Plus
kutoka jijini Arusha, Juma Nature, Imam Abbas, Salu T na msanii matata kutoka
nchni Ghana aitwaye Lucci Mo.
Tamasha
hili, maonyesho ya Swahili Hiphop 2012 pamoja na Swahili Hiphop Summit 2012 yanaletwa
kwenu kwa udhamini wa Ubalozi wa Switzerland nchini Tanzania, Alliance Française
de Dar es Salaam, NSSF, Clouds FM, JD’s Entertainment, gazeti la MwanaSpoti, na
Swahili Hiphop Family Club.
MAHALI: ALLIANCE FRANCAISE DE DAR ES SALAAM
TAREHE: 22 & 23 NOVEMBA 2012 / Kwanzia saa 3asubuh
/ BURE
Mawasiliano: swahilihiphopsummit@gmail.com /
+255 713 300 080
No comments:
Post a Comment