Akizungumza wakati wa semina ya wahariri na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi huo iliyofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya shirikisho hilo , Lyato amesema kuwa baadhi ya wagombea wamekuwa wakigushi vyeti vya elimu na wengine kutumia vyeti vya watoto wao na ndugu zao.
“Tunakumbana na vituko vingi vya ajabu kwenye mchakato wa uchaguzi. Mgombea mwingine amezaliwa mwaka 1952, lakini anakuja na cheti kinachoonesha kwamba amehitimu elimu ya sekondari 1992. Unajiuliza, ilikuwaje?” .
“Baadhi ya wagombea wanakuja na vyeti vya watoto au ndugu zao kwa sababu tu majina yao yanakaribiana. Katika mazingira kama haya, kamati inalazimika kufanya kazi kwa umakini mkubwa kwa sababu tunaamini hakuna kitu kigumu kama kudanganya. Tunawanasa kirahisi sana,” aliongeza.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kamati yake inafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali kuhakikisha kuwa wanapata watu sahihi.
“Kila anayeleta cheti cha elimu, tunawasiliana na shule na vyuo alivyosoma na hata Necta (Baraza la Mitihani la Taifa). Tunafanya hivyo kwa sababu kuna watu wengi wanataka waingie katika uongozi wa shirikisho hili ilhali hawana sifa zinazotakiwa,” .
Katika semina hiyo iliyohudhuriwa na wahariri na waandishi wa habari zaidi ya 40, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah aliwakumbusha wanahabari hao kuhusu uandishi wa habari wenye weledi kuhusiana na uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment