Pilika za usajili wa dirisha dogo zinaendelea kwa kasi, vigogo wakipigana vikumbo kupata wachezaji bora kuziba viraka.
Pamoja na klabu kubwa za Manchester United, Manchester City na 
Chelsea kuzoea kutamba, Tottenham Hotspur inaonesha haikuwa nguvu ya 
soda msimu wa kiangazi.
Spurs walinasa nyota kwa msimu huu, na wanaendelea na jitihada za 
kuimarisha kikosi chao kinachotambia katika tatu bora kwenye msimamo wa 
ligi.
Baada ya kuchelewa msimu uliopita hadi kukosa washambuliaji wa 
kutosha, Liverpool imemsainisha Daniel Sturridge kutoka Chelsea 
kuichezea kwa ‘muda mrefu’ na inamtaraji Tom Ince wa Blackpool.
Joe Cole aliyekuwa yupo yupo Liverpool amejunga na timu aliyoanzia 
akiwa kinda ya West Ham United, ambayo pia imemchukua Marouane Chamakh 
wa Arsenal kwa mkopo hadi mwisho wa msimu.
Luka Modric aliyelazimisha kuondoka Spurs hadi akalimwa faini, sasa 
ana kiu ya kurudi Ligi Kuu ya England (EPL), baada ya kura kuonesha 
ndiye asiyevutia kuliko wachezaji wote wapya wa Real Madrid.
Hivi sasa vigogo wa Manchester United na City pamoja na Chelsea 
wanasemwa kupigana vikumbo kuwania mchezaji huyo mwenye thamani ya pauni
 milioni 33.
Usajili wa dirisha dogo lililo wazi hadi mwisho wa mwezi huu unaweza 
kumaanisha mengi kwa timu zinazowania ubingwa na zile zinazojinasua 
kushuka daraja.
Kimsingi huwa si kipindi cha usajili wa wachezaji wengi, kwani 
inakadiriwa kiasi cha pauni milioni 925 zitatumika ikilinganishwa na 
pauni bilioni 3.685 zilizotumika kati ya Julai na Agosti katika kipindi 
cha miaka 10 iliyopita.
Hata hivyo, klabu zinaweza kujitutumua zaidi kusaini wachezaji 
Januari hii, maana zinajua kuna kitita cha pauni bilioni tatu zinakuja 
Julai kwa ajili ya haki za TV, hivyo kipato chao kitaongezeka.
Spurs wanaofundishwa na Andre Villas-Boas imemtoa bure golikipa wake, Carlo Cudicini kwenda LA Galaxy.
Bado wamebakiwa na makipa mahiri wa kimataifa, Hugo Lloris wa Ufaransa na Mmarekani Brad Friedel.
Wigan iliyo kwenye nafasi tatu za chini ya msimamo imemchomoa mshambuliaji Angelo Henrique wa Manchester United kwa mkopo.
 http://www.tanzaniasports.com/
 
 
 
No comments:
Post a Comment