OFISA
Maendeleo wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) Kusini
mwa Afrika, Ashford Mamelodi amewahakikishia Watanzania kuwa ujumbe wa
Shirikisho hilo utakaokuja nchini mwezi ujao, utafanya uchunguzi wa kina
kuhusu mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (FIFA) na kutoa uamuzi kwa maslahi ya mchezo huo.
“Ninafurahi
kwamba hali ya utulivu imefikia kiwango hiki na nina uhakika FIFA
itafanya uchunguzi wa kina na kufanya uamuzi kwa maslahi ya mpira wa
miguu,” amesema Mamelodi alipokuwa akizungumzia uchaguzi mkuu wa TFF
ambao ulikuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu lakini ukasimamishwa
kutokana na matatizo kadhaa baada ya baadhi ya wagombea kuenguliwa.
Mbali
na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TFF na uchaguzi, safari ya Mamelodi
nchini pia ilihusisha kumtambulisha msaidizi wake, Patrick Onyango
ambaye amejiunga na ofisi hiyo ya FIFA kuanzia mwishoni mwa mwaka jana,
kufuatilia miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na GOAL Project 4 ambayo
ni uwekaji wa nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana na maendeleo ya
Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, mikakati ya mwaka 2013 na kozi
mbalimbali.
Akizungumza
na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Mikutano wa TFF jana, Mamelodi
alisema uamuzi wa Shirikisho hilo kutuma wajumbe katikati ya mwezi ujao
unatokana na mawasiliano baina ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga na FIFA
ambayo ilitaarifiwa hali halisi ilivyo na kama inaweza kusaidia kutatua
matatizo yaliyopo.
“FIFA
haitakuja kuingilia mchakato wa uchaguzi, itakuja kutatua matatizo,”
amesema Mamelodi. “Masuala ya uchaguzi ni ya ndani ya nchi. FIFA haiji
kuichagulia Tanzania rais. Wajumbe wanaweza kumchagua mtu yeyote
wanayeona kuwa anafaa kuwa rais,” amesema Mamelodi.
“Lakini
katiba ya FIFA iko wazi kwamba mwanachama wake ni lazima akubaliane na
sheria za Shirikisho kuwa wanachama ni lazima wabanwe na Katiba ya FIFA.
Kwa hiyo mara tu unapopata uanachama wa FIFA, ni lazima ujue kuwa
utabanwa na katiba ya FIFA na mojawapo ya mambo haya.
“Lakini
kuna tofauti na kitendo cha Serikali kusimamisha uchaguzi kwa kuwa hiyo
inakuwa ni Serikali kuingilia moja kwa moja masuala ya mpira wa miguu,
kitu ambacho katiba ya FIFA inakataza.”
Mamelodi,
ambaye alitumia muda mwingi kuelezea umuhimu wa hali ya utulivu
iliyotawala kwa muda mrefu nchini, amesema anajua kuwa uongozi wa Rais
wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga umefanya mengi katika kuhakikisha
unajenga mazingira mazuri ya maendeleo ya mpira wa miguu, lakini kuna
wakati ni lazima uheshimu uamuzi wa mtu.
“Tenga
amesema imetosha anaondoka na hatuna budi kuheshimu uamuzi wake. Hiyo
ni kauli inayotoka kwa kiongozi wa kweli, kiongozi anayewajibika. Lakini
kwa kuangalia misingi ambayo uongozi wake umeijenga, ni wazi kuwa
kiongozi mpya ataendeleza taasisi bila ya matatizo.
“Tanzania
haikufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, lakini kuna miradi
mingi ya maendeleo ambayo ilifanyika, mingine ambayo ilijaribiwa kwa
mara ya kwanza nchini Tanzania na ikafanikiwa. Kuna Azimio la Bagamoyo,
Semina ya Mawasiliano ya Jamii (Comm-Unity) ya Wanawake, Futuro III na
mingine. Yote hii ilifanyika kwa sababu kulikuwa na utulivu.
“Hivi
sasa TFF ina sekretarieti ina Mkurugenzi wa Ufundi; ina programu za
maendeleo na kuna utulivu. Cha msingi ni kuendeleza haya. Kama mambo
haya yataendelezwa baada ya uchaguzi, ni dhahiri kuwa mpira utazidi
kuendelea. Hakuna njia ya mkato katika maendeleo.”
Uchaguzi wa TFF ulihusisha nafasi za rais, makamu wa rais na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka Kanda 13 za Shirikisho.
Angetile Osiah
Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment