*Ni saa chache baada ya kutwaa ubingwa Afrika
*Tatizo ni fitna za viongozi wa chama cha soka
Kocha wa timu ya soka ya Nigeria, Stephen Keshi amejiuzulu wadhifa huo, saa chache baada ya kuiongoza kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Nigeria walitawazwa wafalme wa soka Afrika Jumapili baada ya kuwafunga Burkina Faso bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Soccer City, Johannesburg.
Sababu kubwa ya kujiuzulu kwa Keshi, ni tetesi kwamba viongozi wa
soka nchini mwake waliacha kumuunga mkono, na wakafikiria kumfuta kazi.
Keshi aliyeichezea Nigeria na kutwaa kombe la AFCON 1994 akiwa
nahodha, alipingwa pia kwa kuacha baadhi ya wachezaji ambao wadau
walidhani wangekuwa muhimu zaidi kwa timu.
Inaaminika kwamba Keshi alitoa notisi na barua ya kujiuzulu kwa Chama
cha Soka cha Nigeria (NFF) muda mfupi tu baada ya kutwaa ubingwa.
Anadaiwa kukabidhi barua hiyo Jumatatu na kuweka bayana uamuzi wake kwa umma, akisema anaamini kwamba amefanya jambo zuri.
“Nimefanya kile ninachoamini ni sahihi kwa kujiuzulu. Niliwapa barua
NFF jana (Jumapili) usiku baada ya sherehe zile,” Keshi amesikika
akiiambia Radio Metro FM.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 51, amechezea Super Eagles mara 51 pia na amepata kubeba mikoba ya ukocha wa timu za taifa za Mali na Togo.
Pamoja na mikingamo aliyokumbana nayo, Keshi ni kocha wa kwanza
mzalendo kutwaa kombe la AFCON kwa taifa lake katika kipindi cha miaka
21, hivyo Nigeria imepata pigo kubwa.
Kwa kujiuzulu kazi aliyofanya tangu mwaka 2011, itabidi ateuliwe
mwingine kwa ajili ya Kombe la FIFA la Vyama vya Soka, ambalo Nigeria
wamefuzu kutokana na ubingwa wao huu, na michuano yake itafanyika majira
ya kiangazi.
Inadaiwa kwamba viongozi wa NFF walituma fedha za nauli ya timu kurudi Nigeria baada ya kupangwa kucheza na Ivory Coast katika robo fainali, tafsiri yake ni kwamba hawakuwa na imani na kocha.
Hata hivyo, Keshi aliwaongoza Super Eagles kuwafunga bao 2-1 Ivory Coast waliokuwa na nyota kama Didier Drogba, Yaya Toure, Cheick Tiote, Gervinho na wengineo.
Keshi amesema wazi kwamba shirikisho hilo la soka lilikuwa likitishia
kumfukuza kazi hata kabla ya mechi dhidi ya Ivory Coast, na kwamba
kitendo cha kuandaa tiketi ni sawa na kumfukuza kazi.
Hata hivyo, Keshi akasema kwamba hakuweka suala hilo akilini mwake wala kuwaeleza watu ili asiivuruge timu.
Uteuzi wa wachezaji aliofanya Keshi, pamoja na jinsi alivyowaongoza
nchini Afrika Kusini, umedhihirisha umahiri wake, kwani umeifufua
Nigeria kimichezo na kutwaa kombe baada ya kulikosa kwa miaka 19.
NFF wanatarajia kujadili barua ya kocha Keshi wakati wowote na
kuitolea uamuzi, lakini mwenyewe anasisitiza kwamba si rahisi abadili
uamuzi wake, kwani NFF wamedhihirisha hawamheshimu yeye wala ujuzi na
uzoefu wake.
Awali, Keshi alinukuliwa awali akisema kwamba angefungasha virago vyake na kuondoka iwapo angebaini kwamba hatakiwi.
Hata hivyo, anasema ni kwa ajili ya uzalendo kwa taifa lake, alibaki
hadi mwisho na kuwaongoza wachezaji hadi kutwaa ubingwa, kisha akaachia
ngazi kwa vile hana uroho wa madaraka.
Keshi, au kwa jina lake kamili, Stephen Okechukwu Keshi alizaliwa
Januari 23, 1962, akacheza mpira katika ngazi ya klabu na hatimaye
taifa.
Katika Afrika, ni yeye na Mahmoud El-Gohary wa Misri tu waliofanikiwa kutwaa kombe wakiwa wachezaji na makocha wa timu zao.
No comments:
Post a Comment