Benchi la ufundi Simba limeongezwa nguvu kwa kuletewa kocha Talib
Hilal anayekuwa wa sita kwa ajili ya kuiandaa timu hiyo kabla ya
kuteremka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza
Jumapili mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya
Recreativo de Libolo ya Afrika Kusini.
Ujio wa Talib ambaye ameshawahi kuichezea timu hiyo na pia
kuifundisha mara kadhaa unawafanya ‘Wekundu wa Msimbazi’ kuwa na makocha
sita wa kiwango cha juu, idadi ambayo pengine ni kubwa kuwahi kuwapo
katika klabu yoyote ya ligi kuu nchini.
Kabla ya ujio wa Talib aliyetua nchini juzi, tayari Simba
ilishakuwa na rundo la makocha ambao ni Mfaransa Patrick Liewig (kocha
mkuu), kocha mkuu wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo 'Julio' (kocha
msaidizi) , Mganda Amatre Richard (viungo), James Kisaka (makipa) na
Mganda Moses Basena aliyewahi pia kuwa kocha mkuu wa Msimbazi lakini
sasa akiwa na cheo cha meneja.
Talib anakumbukwa zaidi pale alipowahi kushirikiana na Mkenya James
Siang'a kuiongoza Simba mwaka 2003 na kuivua ubingwa wa Afrika klabu ya
Zamalek ya Misri na kutinga hatua ya robo fainali. Aliwasili nchini
juzi na leo anatarajiwa kuungana na kikosi hicho kilichoweka kambi ya
muda jijini Arusha.
Talib ambaye anaishi na kufanya
kazi nchini Oman, alisema kuwa amekuja kuongeza nguvu baada ya kutakiwa
kufanya hivyo na uongozi wa klabu hiyo.
Talib alisema kwamba licha ya Simba kutopata matokeo mazuri hivi
karibuni katika mechi zao za ligi, bado anaamini kuwa wana nafasi ya
kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
"Ndiyo nimekuja na jana jioni natarajia kukutana na viongozi
kupanga mikakati mbalimbali. Ila naweza pia nisiende Arusha na timu
ikarejea jijini (Dar es Salaam)," alisema kocha huyo.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alifafanua kuwa Talib
amekuja kuongeza nguvu na wala hachukui nafasi ya Liewig wala kocha
yeyote aliyemkuta klabuni kwao.
Aliongeza kuwa baada ya timu kurejea jijini Dar es Salaam kesho,
wanatarajia kuomba ruhusa ya kutumia Uwanja wa Taifa kabla ya mechi yao
itakayochezwa Jumapili kuanzia saa 10:30 jioni.
Katika hatua nyingine, Simba imekiri kuwa itawakosa Jumapili nyota wake Felix Sunzu na Paul Ngalema wanaosumbuliwa na majeraha.
Daktari wa Simba, Cosmas Kapinga, alisema jana kwamba Sunzu, bado
anamaumivu katika nyama wakati Ngalema aliyeumia goti Jumamosi wakati
wakicheza mechi ya ligi kuu dhidi ya JKT Oljoro, amerejeshwa jijini Dar
es Salaam jana kuendelea na matibabu.
MILOVAN ASOTA
Kocha Mserbia Milovan Cirkovic, ameendelea kuwa na wakati mgumu
jijini Dar es Salaam baada ya viongozi wa juu wa klabu iliyositisha
mkataba wake ya Simba kutoonana naye jana ili kujadili hatma ya malipo
yake kama alivyoahidiwa.
Inaelekea hawataki kuonana nami,” alisema Milovan jana kuzungumzia
ahadi ya kuonana na viongozi wa juu wa Simba, huku akikiri vilevile
kwamba alipigiwa simu na mjumbe mmoja wa kamati ya utendaji Simba na
kuambiwa kuwa asiwe na wasiwasi kwani atalipwa fedha zake (dola za
Marekani 24,000) kupitia akaunti yake.
No comments:
Post a Comment