WATAALAMU
saba wamepitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi
wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) utakaofanyika
Februari 10 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dk. Paul Marealle,
wagombea hao wamepitishwa baada ya kufaulu katika usaili uliofanyika
jana (Februari 5 mwaka huu).
Mwenyekiti
aliyemaliza muda wake Biyondho Ngome anatetea nafasi hiyo dhidi ya
alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Mwanandi Mwankemwa. Nafasi ya Katibu
Mkuu ina mgombea mmoja ambaye ni Nassoro Matuzya wakati nafasi ya
Makamu Mwenyekiti haikupata mgombea.
Sheky
Mngazija ni mgombea pekee wa nafasi ya Katibu Msaidizi kama ilivyo kwa
Juma Mzimbiri aliyepitishwa kuwania nafasi ya Mhazini. Naye Hemed Mziray
ni mgombea pekee wa nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya TASMA.
Nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemvutia Joakim Mshanga pekee.
Wapiga
kura ni wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji na wawakilishi watatu watatu
kutoka mikoa ya Geita, Ilala, Iringa, Kagera, Kinondoni, Mtwara, Rukwa,
Ruvuma na Temeke. Hivyo jumla ya wapiga kura wote ni 33.
No comments:
Post a Comment