By Israel Saria on February 5, 2013
*Mashindano ya FA ni muhimu.
*Mashindano ya mashule yaboreshwe
*Wasomi wa taaluma ya michezo washirikishwe katika maamuzi ya michezo
KILIO cha Watanzania wengi kutaka soka ya Tanzania iinuliwe kilizidi pale Cape Verde
walipofanikiwa kuingia robo fainali ya AFCON. Wanaolia wanahoji, hivi
hawa Cape Verde, moja ya nchi za kiafrika zisizo za soka, wamepandaje
ghafla hivi? Kumbuka, hawa ndiyo walioikwamisha Cameroon kuingia kwenye
fainali hizi. Usishangae hawa wakibeba ubingwa, wamejipanga si kuanzia
sasa bali kuanzia wakati fulani nyuma wakijiwekea malengo wanayoanza
kuyatimiza.
Hawa tuliwafunga kwao 1-0 miaka mitatu tu iliyopita! Kwani ni hawa
tu? Togo nayo imetinga robo fainali. Ni wazi ukiona vyaelea ujue
vimeundwa. Nakukumbusha; mwaka 1994, hawa tuliwafunga kwao 1-0, bao la
winga mwenye kasi wa wakati huo Akida Makunda. Leo wako wapi? Kuleee juu
kabisa kwa kina Nigeria, Ghana, Ivory Coast, Cameroon, Tunisia, Misri na wakubwa wengine wa soka wa bara letu.
Hapo siyo mwisho, Burkina Faso
wanaweza kubeba kombe la AFCON mwaka huu kwa soka kubwa lililoenea
katika kucheza kitimu, kwa nguvu,kwa bidii na akili. Hawa mwaka 2006 na
2007 tu hapa walifungwa na Taifa Stars yetu ya Marcio Maximo kwenye mechi mbili za nyumbani na ugenini. Nyumbani tuliwapiga 2-1 kwa bao la Nizar Khalfan na la kujifunga na kwao tukawalaza 1-0 kwa bao la “video” la Erasto Nyoni. Leo hii hawa si wenzetu kwa sababu wamekuwa watu wa kupanga mambo yao kimkakati, sisi akili zinaishia kwa Yanga na Simba!
Ni vizuri tuwe na sera ya michezo ili tuwe na dira ya tunakotaka
kwenda tukipanga tunaendaje huko na kwa hatua zipi. Ni wazi hii ni siri
ya mafanikio ya Togo, Cape Verde, Burkina Faso na kina Comoro,
Sychelles, Mauritius na wengine. Hili lilishazungumzwa hapa kwa marefu
na mapana ya kutosha.
Kwa tulivyo sasa na mipango yetu hii ya kileo leo kwa ajili ya
mafanikio ya leo leo kupata faida ya leo leo, tunaweza angalau kufanya
kitu fulani cha maana kwenye soka kama wachezaji wetu wataimarishwa
kucheza soka la nguvu lenye ushindani wa hali ya juu huku tukihakikisha
wachezaji wengi wanacheza kupata wigo mpana wa kuchagua wachezaji wa
timu ya taifa na kupata wachezaji wengi watakaouzika nje. Kwa sasa
kikubwa cha soka kinachofanyika nchini ni ligi kuu na vijiligi vya chini
visivyo na msisimko vya timu kupandia kuelekea ligi ligi za juu mpaka
ligi kuu basi. Hatuna mashindano mengine makubwa ya soka ya vilabu.
Kwa mantiki hiyo, kila kocha anatumia kikosi anachokiamini ambacho
kwa mfumo anaoutaka yeye kina wachezaji maalum ambapo kwa mfumo wa
mwingine, wale anaowaweka benchi ndiyo mali zaidi! Na hao wanaokaa
benchi wanaweza wakafanya mambo ya kumfurahisha hata kocha wa timu hiyo
lakini zaidi ya kwenye mazoezi hawana nafasi ya kuonyesha vitu vyao
kwenye soka la ushindani kwani hawapangwi na mashindano pekee tuliyo
nayo ni ligi za madaraja tofauti tu.
Hapa kocha hapaswi kulaumiwa kwani yeye yupo kwa kubeba ubingwa na
si kuwafurahisha wachezaji. Matokeo yake kipa namba moja wa sasa wa
Yanga, Ali Mustafa
“Barthez” alikuwa hachezi kabisa alipokuwa Simba akiwa msaidizi wa kipa
wa Simba Juma Kaseja lakini leo anapocheza akiwa Yanga anaonekana mali
labda hata kumzidi Kaseja wa sasa wa Simba! Amri Kiemba wa Simba, ambaye
kwa sasa nadiriki kusema ndiye kiungo bora wa Tanzania, alishatoswa
vibaya sana na Yanga akikosa namba. Aliokotwa okotwa tu na
wengine lakini alipopata nafasi ya kucheza cheza leo hii ni lulu. Mifano
ni mingi lakini ikitolewa yote hapa, hatutapata nafasi ya kuzungumza
mengine.
Suluhisho la kuwezesha wachezaji wa Tanzania wengi kucheza soka la
ushindani ni kuwa na mashindano makubwa matatu yanayopaswa kufanyika kwa
wakati mmoja ambayo ni ligi kuu ya wakubwa na ligi kuu ya vijana wa
timu za ligi kuu wa chini ya umri wa miaka 21 ambao hawajaingizwa timu
za wakubwa. Ligi ya vijana hawa itakwenda pamoja na ligi za kaka zao na
bingwa kupatikana mwisho wa msimu. Mashindano ya tatu ni ya F.A ya
mtindo wa mtoano ambayo timu zitalazimishwa na mazingira kutumia
wachezaji isiyowatumia mara kwa mara ingawa hazitalazimishwa kikanuni
kutotumia vikosi vile vile vya ligi kuu.
Kwa mfano,kama Simba inacheza na African Lyon
Jumamosi Dar es Salaam kwenye ligi kuu, Jumanne inatakiwa icheze raundi
fulani ya kombe la F.A na Mji ya Mpwapwa mjini Mpwapwa, Dodoma kabla ya
Alhamisi kucheza na Polisi Morogoro
kwenye ligi kuu mjini Morogoro. Hapo lazima itawawajibisha wachezaji
wake wasio katika kikosi cha kwanza kwenye mechi za F.A na hapo ndipo
kina Ali Mustafa na kina Amri Kiemba wangeonekana wakati ule walikuwa na
uwezo mkubwa kiasi gani.
Umuhimu wa mashindano ya F.A ni kupata mechi kali za mtoano za
ushindani za timu za madaraja yote mpaka chini kabisa. Mechi za mtoano
huchezwa kwa juhudi kubwa kuliko za ligi ambapo timu zinazokata tamaa ya
ubingwa, kupata nafasi za juu za uwakilishi kwenye mashindano ya
kimataifa na zenye uhakika wa kutoshuka daraja huzubaa. Kwenye ligi pia
kuna wakati timu huzubaa zikiamini “ligi bado tutaamka tu” lakini kwenye
mashindano ya mtoano,kila timu hupigana kufa na kupona kwani zikizubaa
tu, nje. Kwa sasa Tanzania haina mashindano hata mamoja ya mtoano.
Ratiba yetu ikipangwa vizuri bila kuwepo na mapumziko yasiyo na
tija yoyote ya miezi miwili mizima baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi
kuu yetu kumalizika, tutamudu kuwa na mashindano mengi ya kitaifa na
kimataifa ndani ya msimu. Hapo ndipo tutaibua vipaji vingi mno
vilivyojificha kupitia mashindano hayo mengi na vipaji hivyo vinaweza
angalau kutusogeza mahali fulani katika mipango yetu ya kileo leo. La
muhimu ni kupigana kwa nguvu zote kupata udhamini wa kutosha wa
mashindano hayo mengi kwani ni gharama kubwa kuwa nayo yote. Tunaomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment