UKIINGILIA masuala ya soka per se, unatafuta vita na Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) hata kama wewe ni nani katika nchi yako uliye nje ya uongozi wa soka wa nchi.
Zaidi, wewe ukiwa serikali ndiyo kabisa hutakiwi kuingilia soka ya nchi yako, lakini unaweza kumlipa kocha wa taifa, kulipia kambi ya timu ya taifa, kusafirisha timu ya taifa kwenda nje ya nchi kushiriki mashindano na kadhalika.
Maamuzi ya watu wa soka kwa soka yao usiyaguse hata wakifanya maamuzi
ya ajabu na ya ujinga uliopitiliza! Hivi ndivyo unavyoweza kuyaeleza
kwa ufupi “maagizo” makali ya FIFA kulinda soka yao duniani dhidi ya
dola za nchi.
Kimsingi, soka sasa inaonekana kuwa ni mhimili unaojitegemea wa nchi,
kwani hata ikijadiliwa bungeni maazimio ya Bunge ili yatekelezwe,
lazima utekelezaji huo ufanywe na Serikali au Mahakama wakati Serikali haitakiwi kuingilia masuala ya soka, huku masuala hayo yakiwa hayapaswi kufikishwa wala kuamuliwa mahakamani.
Kwa
msingi huo, mihimili yote ya dola imefungwa mikono kuweka sawa masuala
ya soka yanapovurundwa na kufumbiwa macho na watu wa soka wenyewe au
uvurundaji huo unapofanywa kwa maslahi ya wenye sauti miongoni mwa watu
wa soka.
Katika utaratibu wa mgawanyo wa mamlaka (separation of power)
miongoni mwa Serikali (executive), Bunge (legislature) na Mahakama
(judiciary), kuna utaratibu wa kudhibitiana (check and balance)
ili mhimili mmoja usitumie mamlaka yake ovyo ovyo kwa kujiona hauna wa
kuhoji utendaji wake. Bunge linajadili na kutoa maazimio dhidi ya
serikali na mahakama zinapotenda kinyume, ambapo kwa mahakama si kwa
jinsi zilivyoamua kesi.
Mahakama zinatafsiri sheria za Bunge na kutengeneza misingi mipya ya
kisheria katika kutafsiri huko na zinaamua kesi za utawala dhidi ya
serikali kwa kuweka misingi mizuri ya kisheria ya utawala bora. Serikali
nayo ina mchango katika uongozi wa Bunge kwa kupitia kwa kiongozi wake
bungeni ambaye ni waziri mkuu.
Aidha, Serikali yenyewe ndiyo hupeleka miswada bungeni ya kupitishwa
kuwa sheria. Kwa upande mwingine, Serikali ni mteuzi wa majaji ili
kuhakikisha mhimili wa Mahakama unakuwa na watenda haki walio bora. Kwa
bahati mbaya kwa soka, hakuna udhibiti huo toka mhimili wowote wa dola
baada ya zuio la FIFA kwamba soka isiingiliwe.
Kimsingi, ni sahihi sana kuzuia soka isiingiliwe kwani hali hiyo ingeruhusiwa, mambo
mengi ya soka yangechelewa kwani kila mara, kila chombo kingekuwa
kinakuja na maelekezo yake ya nini kifanyike lini na hata mahakama
zingetumika kusimamisha mashindano kwa amri ya muda (injunction) mpaka
uamuzi fulani utolewe. Hapo hata kalenda za soka zingekuwa matatizoni.
Lakini sasa kinachokera ni kwa maelekezo hayo ya FIFA kutumika Tanzania kana kwamba FIFA hiyo sasa ni rais wetu namba moja anayesaidiwa na namba mbili wake, Jakaya Mrisho Kikwete
katika masuala yoyote yanayogusa utawala wa soka hata kama si ya soka
per se! Mfano wa hivi karibuni ni wa suala la serikali kupinga utaratibu
wa uandikwaji wa katiba mpya ya TFF.
Hili ni suala la kukumbushana kufuata sheria za nchi na si suala la
soka. Kama katiba iliyopo inatengeneza hali ya ulazima (mandatory) wa
katiba mpya kutengenezwa na mkutano mkuu, ikitengenezwa kwa kuipitisha
kwa wajumbe wa mkutano mkuu kuisoma na kuamua (secular resolution)
inakuwa imetengenezwa kinyume cha katiba isipokuwa tu katiba hiyo ikiwa
kimya kwa hilo.
Hata kwa tafsiri ya maneno kwenye katiba, ‘mkutano mkuu’ kwa tafsiri
ya kisheria ni tofauti na ‘wajumbe wa mkutano mkuu’. Mkutano Mkuu ni
mkusanyiko wa mahali fulani na wajumbe wa mkutano mkuu ni watu wanaoweza
kuwa pamoja au walio sehemu mbalimbali.
Katiba ikisema katiba itapitishwa na mkutano mkuu, lazima ipitishwe
na mkusanyiko mmoja wa wajumbe, lakini ikisema itapitishwa na wajumbe wa
mkutano mkuu inaweza kuwa kwa mkusanyiko au kwa kuipitisha kwao
waitolee maoni kwa kuwaendea kokote waliko bila kuwepo mkusanyiko.
Serikali, kupitia mamlaka zake za usajili wa katiba za vyama vya
michezo, inaiona katiba ya chama cha mchezo wa soka imepitishwa kwa
ukiukwaji, inaelekeza ipitishwe kwa taratibu sahihi. Hapo soka
imeingiliwaje na serikali? Nani atarekebisha kosa la TFF la ukiukwaji wa
uandishi wa katiba yao? TFF wenyewe wanaoamini hawakukiuka chochote?
Lazima kuwe na ‘check and balance’ jamani.
Tusifikie mahali pa kuipa FIFA uwezo wa kuwa kama rais wetu katika
masuala yanayohusu watu wa soka. Leo serikali inashughulikia utaratibu
wa utengenezaji wa katiba ya chama cha soka (siyo yaliyomo kwenye
katiba), madai yanatolewa kwamba serikali imeingilia soka. Kesho mtu wa
soka ataiba fedha za chama cha soka, mtasema asichuliwe hatua na vyombo
vya serikali kwa sababu FIFA imezuia serikali kuingilia mambo ya soka na
mwisho mtu wa soka akimuua mwenzake kwenye mkutano wa chama cha soka
mtasema hilo ni suala la soka.
Hebu tuweke mpaka wa mambo ya soka na yasiyo ya soka katika
kushughulikia mambo yetu ya ndani ya nchi, ili tusiipe FIFA urais wa
nchi yetu katika masuala ya soka. Serikali ya Tanzania ipo sahihi
kuhakikisha TFF inapata katiba kwa njia sahihi. Maagizo hayo yapo mbali
na soka kwani hayagusi vipengele vya katiba hiyo.
No comments:
Post a Comment