RAIS
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) amewataka wadau wa
mchezo huo kuwa watulivu kwa vile tofauti zilizojitokeza kati ya
Shirikisho na Serikali zitamalizwa kwa taratibu za mpira wa miguu.
Amesema nia ya TFF ni kuhakikisha Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
haliifungii Tanzania kwani tayari Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alishaahidi kuwepo kikao kati yake na
viongozi wa TFF kitakachofanyika Jumanne (Machi 19 mwaka huu).
“Suluhu
itapatikana kwa mazungumzo kati ya Wizara na TFF. Naamini suala hili
tutalimaliza baada ya kikao cha Machi 19 ambacho kimepangwa na Waziri
kutokana na maombi ya TFF,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa tatizo
lilianzia kwenye mchakato wa uchaguzi ambao umesimamishwa na FIFA.
FIFA
ilisimamisha Mkutano Mkuu wa uchaguzi baada ya baadhi ya wagombea
walioenguliwa kulalamika, na yenyewe kuahidi kutuma ujumbe wa
kushughulikia suala hilo.
Rais
Tenga amesema lisingetokea tatizo hilo, TFF tayari ilishaitisha Mkutano
Mkuu ambao ungefuatiwa na uchaguzi. Lakini kwa vile FIFA ndiyo
iliyosimamisha mkutano huo, TFF inalazimika kusubiri hadi FIFA
itakaposhughulikia suala hilo na kutoa maelekezo ikiwemo lini mkutano
ufanyike.
Amesema
kwa kuamini tatizo hilo litamalizwa ndani ndiyo maana TFF hadi sasa
haijapeleka FIFA maagizo ya Waziri Dk. Fenella ya kutengua marekebisho
ya Katiba ya TFF ya mwaka 2012, kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya
Katiba na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi, kwani ingefanya hivyo Tanzania
ingefungiwa mara moja.
TFF
inasisitiza kuwa FIFA ilijua tatizo la Serikali kutoa maagizo kwake
kupitia vyombo vya habari, hivyo kumuandikia Rais Tenga na kueleza
msimamo wake iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia
uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu.
Uhalali
wa kuwepo kwa barua ya FIFA kwenda kwa Rais Tenga juu ya suala hilo
ulihojiwa pia na mwandishi wa Reuters, Brian Homewood baada ya kusoma
kupitia vyombo vya habari nchini kuwa Shirikisho hilo huenda likaifungia
Tanzania ikibainika Serikali inaingilia shughuli za TFF. Mawasiliano
kati ya FIFA na mwandishi huyo ambapo majibu yake pia TFF ilipewa nakala
yameambatanishwa katika taarifa hii.
No comments:
Post a Comment