HABARI MPENZI MWANAMICHEZO KARIBU KATIKA KURASA HII MAHSUSI KWA HABARI ZA MICHEZO PIA UNAWEZA KUTANGAZA BIASHARA YAKO HAPA KWA BEI NAFUU ZAIDI KWA MUDA MREFU ZAIDI WASILIANA NASI KWA NAMBA +255713 15 33 48

17 April 2013

HUYU NDIYE MAREHEMU BI KIDUDE AMBAYE MUNGU KAMPENDA ZAIDI SIKU YA LEO


Bi Kidude ni msanii mkongwe na mahiri sana katika fani ya muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.


Bi Kidude.png
Mwanamuziki mkongwe katika Taarab Fatuma Bint Mbaraka maarufu kwa jina la Bi Kidude amefariki dunia muda mchache uliopita huko Bububu Zanzibar, sehemu alikokuwa anaugulia kwa kipindi sasa. Mwili wake utahamishiwa kwake Rahaleo na mazishi yatakuwa kesho. Bi Kidude alizaliwa katika kijiji cha Mfagimaringo, alikuwa binti wa mchuuzi wa nazi, hakuna anayejua haswa Bibi huyu alizaliwa tarehe ngapi, kuna hata mawazo kuwa alikwishafikisha miaka 102.
Katika mwaka 1920 tayari alikuwa amekwisha anza kuimba katika vikundi vya sanaa kule kwao, mwaka 1930 alijiunga na Egyptian Musical Club ya Dar es Salaam na kuzunguka miji mingi ya Tanganyika wakati ule , mwaka 1940 alirudi Zanzibar ambako awali alikuwa amekimbia kwa kuwa aliozwa kwa nguvu na mtu aliyemzidi sana umri.

 
 Bi Kidude pia aliwahi kuimba na Sitti Binti Sadi wakati wa ujana wake, na katika maisha yake Bi Kidude amekwisha zunguka mabara yote akiimba katika majukwaa na wanamuziki maarufu ulimwenguni
Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar. Bi Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya. Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
 
Bi Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti binti Saad
Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko 
aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
Bi Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya 'wanja' na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
 
Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Kurani.
Mungu Amlaze Pema Peponi Bibi yetu. Amen

No comments:

Post a Comment

lisungu_chisara@yahoo.com

TUTUMIE HABARI YOYOTE YA MICHEZO, BURUDANI TUTAZICHAPISHA

TANGAZA KWA MFUMO HUU


MAHUDHURIO YA WASOMAJI KIMATAIFA

free counters

Followers