Baadhi
ya wanachama wa klabu ya Pan African wameushtaki uongozi wao kwa Chama
cha Soka Wilaya ya Ilala (IDFA) kwa madai ya kukiuka katiba yao ikiwa ni
pamoja na kushindwa kuitisha mkutano mkuu tangu walipoingia madarakani
mwaka 2009.
Kwa mujibu wa barua yao kwenda ya Machi 30, 2012 kwenda kwa katibu
mkuu wa IDFA, wanachama hao wamedai kuwa tangu uongozi wao ulipoingia
madarakani Aprili 18, 2009, haujawahi kuitisha mkutano wowote wala
kushirikisha wanachama katika maamuzi yoyote yale ya klabu.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na mmoja wa wanachama wa klabu hiyo
aitwaye Abbas Ally (mwenye kadi namba 0075), imedai kuwa klabu hiyo pia
imekuwa haina ofisi ingawa ina jengo lake la ghorofa.
"Jambo jingine linalotutisha ni klabu kutokuwa na ofisi yake. Tuna
jengo letu ambalo uongozi umelipangisha lote na wanachama tunakosa
mahali pa kupata huduma za klabu au kupata taarifa na kulipia ada za
uanachama," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Wanachama hao wameiomba IDFA kuushinikiza uongozi kuitisha mkutano
wa wanachama na wao (IDFA) wakiwapo kushuhudia, huku wakiongeza kuwa
miongoni mwa mambo ya kujadiliwa yawe ni ripoti ya mapato na matumizi
kwa kipindi chote walichokaa madarakani na sababu za kupangishwa kwa
jengo lao lote huku klabu ikikosa ofisi.
Makamu Mwenyekiti wa Pan, Ally Hemed, amesema kuwa
asingeweza kuzungumzia madai ya wanachama na badala yake akataka
atafutwe katibu mkuu wao, Saad Mateo. Mwandishi hakuweza kumpata katibu
huyo na jitihada za kuwasiliana naye kupitia simu zake zilishindikana
pia kwa vile zilikuwa hazipatikani.
Katibu Mkuu wa IDFA, Daud Kanuti, alithibitisha kupokea barua ya
wanachama wa Pan na kusema kuwa walishaamua kuzikutanisha pande zote ili
kujadili masuala ya klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment