Sheria mpya ya shirikisho la mpira wa mikono la kimataifa (IHF) ya
mchezaji kupewa kadi nyekundu na kufungiwa mechi moja pale anapotenda
kosa kubwa wakati wa mchezo itaanza kutumika rasmi katika Ligi ya
Muungano ya mchezo huo itakayoanza Aprili 20 katika uwanja wa ndani wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Kupitishwa kwa sheria hiyo mpya kulikuja mwaka 2010, lakini kwa
upande wa Tanzania itaanza kutumika rasmi katika Ligi ya Muungano baada
ya wachezaji, makocha na waamuzi kupewa semina kuhusiana na sheria hiyo.
kaimu katibu msaidizi wa chama cha
mpira wa mikono nchini (TAHA), Joseph Muhagama amesema awali ilikuwa
mchezaji akifanya kosa uwanjani, alikuwa anatolewa nje kwa muda wa
dakika mbili na baadae anarejea tena uwanjani.
Alisema kwa mujibu wa marekebisho yaliyofanywa na IHF, sheria hiyo
sasa inamfanya aliyepewa kadi nyekundu kutoka moja kwa moja kwenye mechi
na kufungiwa mechi moja.
Aliongeza kuwa tayari chama cha mchezo huo cha Zanzibar (ZAHA) na
TAHA wamekubaliana sheria hiyo ianze rasmi katika mashindano hayo
yanayoshirikisha timu za Bara na Visiwani zilizoshika nafasi ya juu
katika mashindano ya klabu bingwa ya taifa.
Alizitaja timu zitakazoshiriki katika mashindano hayo kwa upande wa
bara kuwa ni Ngome, Magereza, JKT na Mpwapwa Star, wakati kutoka
visiwani ni JKU, Nyuki na Mwanakwerekwe, zote zikiwa za wanawake na
wanaume.
Katika hali nyingine, Muhagama aliwataka wagombea nafasi mbalimbali
katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 26 jijini Dar es
Salaam kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu pale zitakapoanza kutolewa na
Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
No comments:
Post a Comment