NIMEKUWA nikiguswa sana na kilio kinachotolewa na katibu mkuu wa
Chama cha Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui, ambaye haishi
kuwapigia magoti wadau wa michezo na wafanyabiashara kuwaomba udhamini
kwenye mchezo huo.
Jambo moja lililonisababisha kuguswa na kilio cha Nyambui ni namna
ambavyo yeye pekee anavyohangaika kuomba udhamini huo huku viongozi
wengine akiwemo mwenyekiti wa RT, Francis John, wakiwa hawasikiki.
Binafsi ninamfahamu kidogo Nyambui ambaye aliwahi kuwa mvuvi katika
wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza kabla ya chama cha riadha mkoa wa Mwanza
wakati huo kukiona kipaji chake na kuamua kukiendeleza.
Nyambui ambaye February 13 mwaka huu atakuwa anatimiza miaka 59, ama
kwa kujua adha wanazopata vijana wengi walio kwenye mchezo wa riadha au
kwa kutaka kuona vijana wengi wanafuata nyayo zake amekuwa akikubali
kudhalilika ili mradi riadha Tanzania isimame upya.
Riadha imeshindwa kuwika tangu kumalizika kwa enzi za kina Filbert
Bayi na baadaye kina Nyambui ambaye aliwahi kushinda medali ya fedha
katika mbio za mita 5,000 mwaka 1980 kwenye michezo ya Olimpiki na
baadaye kushinda medali ya shaba katika michuano ya All African Games na
mara mbili 1987/88 Berlin Marathon.
Nadhani kama viongozi wote wa riadha wangejitokeza kila kukicha
kuyapigia magoti makampuni pamoja na wadau wengine wa michezo huenda leo
hii kungekuwa na wadhamini wengi kama ilivyo kwenye soka.
Kwa nchi kama Tanzania ambayo kuna makampuni makubwa ambayo yanapaswa
kujitangaza kupitia michezo hayafanyi hivyo kutokana na kukosa mguso;
nimeona vema niwakumbushe Watanzania wenzangu kuwa tukijitosa
hatumsaidii Nyambui bali riadha ya Tanzania.
Hivi sasa vijana wetu wanajiandaa kwa ajili ya michuano ya Olimpiki
London tukiweza kuchangia kuiweka timu kambini na wakafanikiwa kupata
medali itakuwa sifa ya taifa na tutatembea kifua mbele sote.
Kama zilivyomwagiwa misaada timu za soka, ikifanyika hivi na kwenye
riadha ninaamini kuwa Tanzania inaweza kuwika na kuzipiku Kenya,
Ethiopia na Morocco ambazo kwa sasa zimekuwa zikifanya vema katika
medani ya michezo barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Inasikitisha kuona kuwa kambi ya timu ya taifa ya riadha inasubiri
majaaliwa huku vijana wakisubiri maandalizi ya kusadikika, hawajui
yataanza lini wakati wenzao wa nchi nyingine wakiendelea kujifua.
Kwa upande mmoja nadhani serikali yetu imechangia kwa kiasi kikubwa
haya yanayotokea katika riadha kwa kuwa haionyeshi kuwajali hata
wanariadha walioliletea sifa taifa mfano Filbert Bayi au hata Jonh
Stephen Akwari ambaye kajengewa mnara wenye sanamu yake nchini China
lakini hapa Tanzania hakuna anayemjua tena.
Hakuna ubishi kuwa Tanzania inavyo vipaji vingi vya riadha ambavyo
vingeweza kutamba kimataifa lakini havijitokezi kwa kuwa
havijahamasishwa na ili hamasa ionekane, ni kuanza kwa kuwawezesha hawa
waliopo sasa.
No comments:
Post a Comment