HADITHI zisizokwisha za ukosefu wa fedha kwa timu zetu za taifa
pale zinapokabiliwa na michuano ya kimataifa zitamalizika pale tu
tutakapoamua kama taifa kujiondoshea aibu hiyo.
Limekuwa ni jambo la kawaida kabisa kuwasikia viongozi wa timu za
taifa za michezo mbali mbali kupiga kelele za kuomba fedha kutoka kwa
watu binafsi na makampuni kila mara wanapokabiliwa na mashindano.
Hii ni kwa sababu hakuna utaratibu wa serikali kupitia Wizara ya
Michezo kuweka fungu kwa ajili ya timu za taifa za michezo mbalimbali.
Mfano mzuri ni ujio wa michuano ya Afrika kwa mchezo wa netiboli
ambayo inatarajiwa kufanyika nchini mwezi ujao, lakini jambo la
kushangaza ni maandalizi duni kwa timu yetu ya taifa achilia mbali
maandalizi ya uenyeji kwa ujumla.
Viongozi wa Chama cha Netibali Tanzania (CHANETA) wamepiga kelele
mpaka wamechoka kuomba msaada wa fedha za kuwawezesha kuiandaa timu
pamoja na fedha kwa ajili ya maandalizi ya mashindano kwa ujumla.
Binafsi ninaamini kuwa utaratibu wetu katika kukusanya fedha kitaifa
kwa ajili ya michezo sio mzuri ndiyo maana hivi karibuni mke wa Waziri
Mkuu, mama Tunu Pinda, alifikia hatua za kuiombea CHANETA misaada kutoka
kwa Watanzania.
Binafsi naona baada ya CHANETA kupewa uenyeji huo na Chama cha
Netiboli Afrika, serikali ilipaswa kulibeba hilo na kulifanya kuwa
jukumu lake hivyo kutoa fedha za maandalizi ya mashindano kwa ujumla na
fedha za kuiandaa timu ya taifa.
Ingawa pia ninaweza kuilaumu CHANETA kwa kukubali uenyeji wa
mashindano makubwa kama haya wakati inafahamu fika kwamba haina fedha
mfukoni zaidi ya kutegemea fedha kutoka kwa wadau watakaoguswa, lakini
ni ukweli usiopingika kwamba iwapo wadau hawatajitokeza tutaaibika.
Aibu hii haitakuwa ya CHANETA peke yake bali ya taifa zima, iwapo
wageni watakuja wakakosa mahali pa kufikia au wakakosa chakula kutokana
na wenyeji wao kutokuwa na fedha za kuwakirimu kulipia hoteli.
Ingawa sifahamu taratibu zao kama kila nchi inajigharamia au vipi,
lakini ikiwa zinategemea mfuko wa wenyeji kwa hakika hali itakuwa mbaya
sana.
Kwa kuwa suala hili la ukata limekuwa likijitokeza katika kila mchezo,
nadhani sasa tumejifunza na tunaweza kulifanya sasa kwa faida ya
Tanzania na wananchi wake kwamba tunaweza kuanzisha mfuko maalumu wa
michezo utakaochangiwa na kila mwananchi.
Hii itasaidia timu za taifa kujiandaa kikamilifu na vyama kuomba
uenyeji wa michuano yoyote ya kimataifa kwa sababu hawatakuwa na hofu ya
kuifanikisha na hapo wachezaji wetu watapata nafasi ya kutamba
kimataifa.
Tukiangalia jinsi wachezaji wetu wanavyofanya vibaya kulinganisha na
wenzetu wa nchi jirani tutaona kwamba huu ni muda muafaka wa kufanya
uamuzi wenye manufaa kwa taifa.
Bila ya serikali kuweka mpango utakaowawezesha Watanzania wote
kuzichangia timu zao kabla ya kuanza kwa michuano kupitia mfuko maalumu
wa michezo, nchi yetu itaendelea kuwa msindikizaji katika michezo.
Binafsi niliumia sana nilipowashuhudia wanariadha wa Kenya waking’ara
katika mashindano ya Kilimanjaro Marathon ambapo waliweza kutwaa medali
zote tangu kwa wanawake hadi kwa wanaume na sisi kuishia kumwaga
visingizio.
Binafsi sioni sababu ya kutufanya Watanzania tushindwe kufanya vizuri
katika michezo ya kimataifa wakati tunavyo vipaji vya kila namna kama
wanavyotuambia siku zote wataalamu kutoka nje pindi wanapozulu nchini
ambapo husema Tanzania imejaliwa vipaji isipokuwa vinakosa kuendelezwa.
Naamini tukiweza kuanzisha mfuko wetu wa maendeleo ya michezo
isingewezekana kwa CHANETA kufikia hatua ya kumuomba mke wa Waziri Mkuu
awapigie debe ya kuomba fedha za maandalizi ya timu au ya mashindano
makubwa kama haya.
Tunapaswa kuanzisha mfuko huo sambamba na kuanza kuziandaa timu za
vijana za chini ya miaka 20 za michezo mbali mbali tangu sasa, kwa
kuweka malengo ya kucheza miaka mitano ijayo.
Mfano katika soka tunapaswa kuanza kuiandaa timu itakayoshindana na
kuwa na uwezo wa kushinda Kombe la Mataifa Afrika 2017, 2019, 2021 na
Kombe la Dunia mwaka 2022, litakaloandaliwa katika nchi ndogo ya Qatar
na hali kama hiyo pia iwe ndiyo lengo kwa michezo mingine.
No comments:
Post a Comment