Timu ya taifa ya kuogelea inaanza harakati za kutafuta tiketi ya
kufuzu kushiriki kwenye michuano ya dunia itakayofanyika Agosti mjini
Barcelona, Hispania kwa kutupa karata yake katika michuano ya awali
mjini Lusaka, Zambia leo.
Kikosi cha waogeleaji 18 na kocha mmoja kiliondoka jana asubuhi
jijini Dar es Salaam kwenda Lusaka tayari kwa michuano ya Afrika
inayoanza asubuhi ya leo nchini humo.
Nahodha wa timu hiyo, Hilal Hilal alisema jana kabla ya kuondoka
Dar es Salaam kuwa wanakwenda kushinda na si kushiriki na akasisitiza
kwamba licha ya timu yao kuwa na rekodi ya kufanya vibaya kwenye michezo
ya Olimpiki na Afrika wana mategemeo ya kutwaa medali kwenye michuano
hiyo.
"Tumefanya mazoezi ya kutosha chini ya kocha John (Belela),
tunategemea hatutamwangusha na pia tutaitangaza vyema nchi yetu kwa
kutwaa medali," alisema Hilal.
Kocha wa timu hiyo, Belela alisema wana mategemeo makubwa ya
kushinda japo timu za Afrika Kusini na Zimbambwe zinawapa presha kwakuwa
nchi hizo zina miundombinu bora ya mchezo huo kulinganisha na
Tanzania.
Belela alisema mbali na mataifa hayo, hakuna nchi nyingine
wanayoihofia na kwamba timu yake itafanya vizuri kwa kurejea na medali
na pia kufuzu kushiriki mashindano ya dunia.
Kwa mujibu wa mkuu wa msafara wa timu hiyo ambaye pia ni katibu
mkuu msaidizi wa chama cha kuogelea Tanzania (TSA), Ramadhani Namkoveka,
jumla ya nchi 17 zitashiriki kwenye michuano hiyo.
Namkoveka alizitaja nchi hizo kuwa ni Botswana, Zimbabwe, Afrika
Kusini, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Madagascar, Shelisheli, Angola,
Namibia na wenyeji Zambia.
Aidha, aliwashukuru wadhamini wa timu hiyo ya taifa Bay Port
Finance Services na MarryBrown kwa kusaidia kufanikisha safari hiyo.
Wachezaji walioondoka ni pamoja na Hilal Hilal, Adam David, Sonia
Tumiotto, Sakura Ito, Amaar Ghadiyali, Iyas Shivji, Malindi Vaughan,
Anjani Taylor, Matthew Guild, Emma Imhoff, Sabrina Kassam, Mubanga
Peeperkorn, Mariam Foum, Mohamed Said, Alizee Bollen, Shammrad
Magesvaran, Smriti Gokarm, Dhashrrad Magesvaran na Catherine Mason.
No comments:
Post a Comment