LIGI
kuu ya soka Zanzibar, inaingia katika hatua ya mwisho zikiwa zimebaki
mechi chache kwa kila timu kumaliza msimu wa mwaka 2012/13.
Hata hivyo, inasikitisha kuwa, ligi hiyo inamalizika kwa staili ya kushangaza ambayo mtu hawezi kuikuta katika nchi yoyote duniani.
Katika hali ya kawaida, ligi za soka katika nchi zote zenye mipango makini duniani, huenda sawa kwa kila timu kucheza idadi sawa za mechi.
Hii ina maana kuwa, hata siku ya mwisho, timu zote huwa zinashuka katika viwanja tafauti ili kumaliza mechi zao za mwisho hata kama mara nyengine hutokezea bingwa kupatikana kabla siku hiyo kulingana kwa wingi wa pointi na mazingira yalivyo katika msimamo.
Lakini, katika miaka ya karibuni, ligi kuu ya Zanzibar imekuwa haina historia ya kwenda kwa hesabu kama hizo, hali inayodhihirisha kwamba chama hicho hakizingatii umuhimu wa timu zinazoshiriki kutokupishana kwa idadi kubwa ya mechi walizocheza.
Kwa hiyo, si ajabu kukuta siku ya mwisho ya ligi hiyo, kunakuwa na baadhi ya timu zisizokuwa na michezo kwani huwa zimeshamaliza kitambo, huku tamati ya ligi ikihusisha baadhi ya timu tu.
Hali kama hii ndiyo inayotoa nafasi kwa timu nyengine zinazoweka maslahi mbele, kukubali kuingia makubaliano kwa kuuza na kununua mechi, na hivyo kupata matokeo yanayozibeba baadhi ya timu hata zile ambazo hazishuki viwanjani siku ya mwisho.
Daima wadau na vyombo vya habari, vimekuwa vikipaza sauti kueleza umuhimu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kuendesha mambo kitaalamu ili ligi zake ziende vizuri na kwa kuzingatia uwiano wa mechi badala ya mtindo wa sasa.
Pamoja na ZFA kutia pamba masikioni kwa kutotaka kubadilika katika hili, bado ukweli unabaki kwama chama hicho kinahitaji kuendeshwa kitaalamu kwa kushirikisha watu makini na wenye ufahamu wa kupanga ratiba ambazo hazitakuwa zikitiwa mikono mara kwa mara bila ya sababu za msingi.
Haiingii akilini kwamba ligi inakaribia kwisha huku kukiwa na timu zilizobakiwa na michezo sita, nyengine mitano na baadhi mitatu.
Huku ni kuzipa mwanya timu kutengeneza matokeo na kamwe ZFA haitakuwa na haki ya kuzihukumu iwapo hilo linatokea kwani yenyewe ndiyo iliyoshindwa ulezi.
Kwa namna hii ambayo ZFA inaendesha ligi zake, sifikirii kama kuna njia yoyote ya kuepuka upangaji matokeo, kwani ziko timu hata ushindi katika mechi za mwisho hauziongezei kitu kwani haiziwezi kupata ubingwa wala kushuka daraja.
Mara kadhaa chama kimekuwa kikijigamba kuwa kitakuwa makini kuhakikisha rushwa haijipenyezi katika ligi zake, lakini majigambo hayo ninayaona sawa na nguvu ya soda kwani imebainika kuwa baadhi ya viongozi wa chama hicho wenyewe wanalea hali hiyo kwa kuwa na timu wazipendazo au za sahibu zao.
Aidha, mara nyengine, mazingira ya kuuza mechi huonekana wazi wazi viwanjani, lakini hatusikii hatua zinazochukuliwa kuwaadabisha wahusika, kwani muhali na urafiki ndivyo vinavyotawala katika suala zima la kusimamia mpira wa miguu nchini.
Ushahidi wa ZFA kuwa na viongozi wenye timu zinazoshiriki ligi si jambo la siri kwani imewahi kutokea hapo nyuma, mmoja wa wajumbe wa kamati tendaji kuelezewa alimrubuni mchezo mmoja akiri kuwa saini aliyoiweka katika kadi yake ya usajili wa timu nyengine si yake.
Sasa, kama hali iko hivyo, haitakuwa ajabu siku ya mwisho ya ligi kuu, tukashuhudia matokeo ya kupangwa kwani nafasi hiyo nina hakika itakuwepo na bila shaka baadhi ya timu hazitaiacha kwani hakuna iliyo tayari kushuka daraja kirahisi.
Hali kama hiyo pia ndiyo mara nyengine inayotufanya tupate bingwa wa kuandaliwa ambaye hata ushiriki wake kwenye mashindano ya kimataifa unakuwa wa kushindikiza timu pinzani na usiokuwa na ushindani.
Aidha, kwa kutumia fedha, ziko timu zitaepuka kushuka daraja na zile pangu pakavu, zitajikuta zikididimia na kutoa mkono wa buriani katika ligi kuu na kwenda kucheza ligi daraja la kwanza.
Naam, fedha sabuni ya roho, na wengine husema 'Penye udhia penyeza rupia', tusubiri kuona hatima ya ligi kuu itakavyokuwa.
Jengine linaloifanya ZFA ionekane imechoka, ni jinsi ilivyopanga ratiba kiasi cha timu moja ya Unguja kupangiwa kumaliza mechi zake nne kati ya tano ilizobakisha kisiwani Pemba .
Bila shaka hali hiyo inaifanya timu hiyo ikabiliwe na mazingira magumu kuondoka na pointi hasa ikizingatiwa kuwa nayo inatapia roho na baadhi ya timu za huko katika kukimbia hatari ya kushuka daraja.
Katika namna hii ya upangaji ratiba, mara nyingi ZFA hutoa kisingizio cha kukosekana viwanja vya kutosha, na pia umasikini wa timu za Zanzibar ambazo kwao ni mzigo mzito kusafiri mfululizo kutoka kisiwa kimoja hadi chengine.
Hata kama hizo zaweza kuwa sababu za msingi, bado ZFA haiwezi kujivua dhima ya upangaji matokeo endapo utatokea, na ninaamini utafanyika kwani haya ni mazoea katika ligi zetu na sio kama ninashawishi lifanyike.
Katika nchi nyingi duniani, mechi za mwisho za ligi hutarajiwa ziwe na msisimko mkubwa na ushindani wa hali ya juu kwani, ukiondoa baadhi ya timu zilizoshuka daraja mapema, ziko nyengine huwa hazijijui na pia hutegemea matokeo ya mechi nyengine mbali na zile zinazocheza zenyewe.
Lakini ni masikitiko makubwa kwamba hapa kwetu hali haiko hivyo, na ninathubutu kusema kwamba hili husababishwa na mfumo mbovu wa upangaji ratiba na namna ya kuitekeleza.
Kwa hivyo, wakati ligi kuu ikielekea mfundani, lazima ZFA ikubali kuwajibika kwa matokeo ya kupangwa yatakayojiri viwanjani siku ya mwisho ya ligi hiyo kwani yenyewe ndiyo iliyopanda mzizi huo.
No comments:
Post a Comment