CHAMA cha Soka Zanzibar, kimepata Rais mpya kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika leo katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Aliyefanikiwa kukalia kiti hicho, ni
Ravia Idarous Faina (42), aliyewabwaga wapinzani wake wawili, kwa kuzoa
kura 37 kati ya 53 zilizopigwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa ZFA.
Abdallah Juma Mohammed, Mwanasheria wa chama hicho, yeye alipata kura
16, huku mwanafunzi anayetarajia kuhitimu digrii ya sheria katika Chuo
Kikuu cha Zanzibar Tunguu , Rajab Ali Rajab akishindwa
kupata hata kura moja.
Uchaguzi huo uliitishwa kufuatia
kujiuzulu kwa Amani Ibrahim Makungu mwishoni mwa mwezi Januari mwaka
huu, baada ya kukiongoza chama hicho kwa miezi saba tu.
Makungu pia alichukua nafasi hiyo
kupitia uchaguzi mdogo uliofanyika Juni 30, 2012, baada ya kuachia ngazi
kwa Ali Ferej Tamim, aliyekaa madarakani kwa zaidi ya miongo miwili.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa
matokeo hayo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho Gulam
Abdallah Rashid, Rais huyo mpya aliwashukuru wote waliomchagua na
waliomnyima kura, na kusema ushindi huo ni wa kila anayelitakia mema ZFA
na soka la Zanzibar.
, kila uchaguzi unakuwa na mambo
yake, pamoja na wagombea kubebwa na watu wanaowaunga mkono, lakini
mwisho mshindi anakuwa mmoja, hivyo wapiga kura wanapaswa kuvunja kambi
zao ili kuimarisha chama na kufanya kazi kwa matakwa ya Wazanzibari.
Aliahidi kuongoza kwa kufuata katiba na
kanuni zinazotawala mpira wa miguu Zanzibar , na kusema hatakaribisha
nafasi ya uongozi au utendaji isiyotajwa ndani ya katiba.
Aidha, alisema kwa wakati wote akiwa
madarakani, atahakikisha chama kinakuwa na sauti ya pamoja na kuvunja
mgawanyiko kati ya Unguja na Pemba ( UFA na PFA) yaani Unguja Football
Association na Pemba Football Association kama wengi walivyoanza
kubatiza.
Mpinzani wa karibu wa Ravia, Abdallah
Juma Mohammed alimpongeza mshindi huyo na kusema amekubali matokeo na
namna Kamati ya Uchaguzi ilivyoendesha zoezi hilo .
“Uchaguzi ni mchezo wa kubahatisha, yawezekana wapiga kura wamevutiwa
zaidi na sera za mgombea mwenzangu na hivyo kumpigia kura nyingi. Hata
hivyo ninaahidi kumsaidia kwa ushauri na lolote atakalotaka kwa manufaa
ya soka letu,” alieleza.
Naye Rajab Ali Rajab ambaye hakuambulia
kura yoyote, alikiri kuwa uchaguzi umefanyika vizuri, ingawa alionesha
wasiwasi kuwa huenda wapiga kura ZFA wanaangalia zaidi sura na umaarufu,
na sio sera za wagombea.
Alisema idadi ndogo ya wapiga kura,
inachangia kushawishi kurubuniwa, na hivyo mshindi kupatikana kwa namna
anavyokunjua mkono wake.
Mwenyeikiti wa Kamati ya Uchaguzi Gulam
Abdallah Rashid, aliishauri ZFA kuwa makini katika maandalizi, na
kuepuka kasoro zinazosababisha usumbufu ikiwemo kuchelewa kuipa kamati
yake taarifa muhimu.
Ravia anakuwa Rais wa tatu ndani ya
kipindi kimoja cha uchaguzi ambacho uongozi wake hudumu wa miaka minne,
akitanguliwa na Ali Ferej Tamim na Amani Ibrahim Makungu waliobwaga
manyanga kwa sababu mbalimbali.
No comments:
Post a Comment