Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchaguzi ili kufanya uamuzi wenye manufaa kwa washabiki wa mpira wa
miguu baada ya tarehe ya uchaguzi aliyotangaza kuingilia na mechi ya
watani wa jadi (Simba na Yanga) ya Ligi Kuu ya Vodacom.
Sekretarieti
ya TFF imepokea maoni kutoka kwa wapenzi mbalimbali wa mpira wa miguu
wakiomba matukio hayo mawili (Uchaguzi wa TFF na mechi ya Simba na
Yanga) yafanyike katika siku tofauti.
Wakati
Kamati ya Uchaguzi inatangaza uchaguzi kufanyika Oktoba 20 mwaka huu
tayari ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ilikuwa imeshatoka, na ikionesha
kuwa timu ambazo zina historia ya kipekee katika mpira wa miguu
zitacheza siku hiyo.
Sekretarieti
imelazimika kumwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kwa vile yeye
na kamati yake ndiye wenye mamlaka ya kuitisha Mkutano wa Uchaguzi. Huko
nyuma TFF imeshafanya mikutano huku kukiwa na mechi za timu ya Taifa
(Taifa Stars), jambo ambalo liliwezekana kutokana na mikutano hiyo kuwa
na ajenda moja tu.
Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ameitisha kikao cha kamati yake kujadili barua hiyo ya sekretarieti.
No comments:
Post a Comment