Ligi Kuu ya England (EPL) imeanza na zogo kubwa ni kichapo walichopokea Arsenal cha mabao 3-1 nyumbani, kutoka kwa Aston Villa.
Juu ya hilo, ni kushindwa kwa klabu hiyo kubwa kusajili nyota wapya,
licha ya ahadi kemkem kwamba walishajiandaa kutumia kitita kuongeza
nguvu, hasa kwenye ushambuliaji.
Hakuna wasiwasi kwamba Arsene Wenger ni mmoja wa makocha bora kabisa ambao EPL imepata kuwa nao, lakini mkakati wake unaonekana kupitwa na wakati.
Ni kana kwamba anaona kufanya usajili mkubwa na wa kutikisa kama
kushindwa na si mafanikio, na ndilo linaweza kuwa jibu pekee la yeye
hadi sasa kusajili tu kijana mdogo Yaya Sanogo kutoka Auxerre badala ya nyota wanaotakiwa.
Bodi ya Wakurugenzi ya Arsenal imetamka wazi kwamba wana fedha za
kusajili na walikuwa tayari kupigana vikumbo na klabu nyingine kubwa
kwenye usajili, lakini siku zinayoyoma hakuna vitendo.
Pauni zote milioni 70 zilizosemwa zimetengwa pamoja na nyingine zilizopatikana baada ya kuuza wachezaji kadhaa na wengine kutolewa kwa mkopo zimewekwa kibindoni tu.
Washabiki wa Arsenal tayari wamebwatuka kwamba hawataki tena Mfaransa
huyo aongezewe muda, pindi mkataba wake utakapomalizika mwakani.
Hawawezi kuridhika na madai ya Wenger kwamba walitaka kumsajili Gonzalo Higuain,
Luis Suarez na hata Wayne Rooney, kwa sababu dili kama la Higuain
ilielekea wazi waliliacha likayeyuka akachukuliwa na klabu nyingine.
Suarez inaeleweka msimamo mkali wa mmiliki na viongozi wa Liverpool,
lakini Arsenal walitakiwa kujua asingeachiwa kirahisi, hivyo
wangeangalia na kukomaa kupata nyota wengine.
Walifanya mzaha tu kwa wengine kama akina Bernard na Luiz Gustavo – ambapo Gustavo kutoka Bayern Munich alisema wazi alitaka kujiunga Arsenal, lakini Wenger akakunja mikono yake badala ya kuinyoosha kumpokea.
Walifanya mzaha tu kwa wengine kama akina Bernard na Luiz Gustavo – ambapo Gustavo kutoka Bayern Munich alisema wazi alitaka kujiunga Arsenal, lakini Wenger akakunja mikono yake badala ya kuinyoosha kumpokea.
Wapinzani wao waliomaliza ligi juu yao wote wana vikosi imara lakini
wameongeza wachezaji kadhaa au hata mmoja kama Manchester United.
Waliomaliza nyuma yao pointi moja, Tottenham Hotspur wamejiimarisha
vilivyo, na tusishangae msimu huu wakawatimulia vumbi mahasimu wao hao
wa London kaskazini.
Spurs wamewasajili mpachika mabao mahiri, Roberto Soldado na kiungo
Paulinho na kuna mwingine pia wanadaiwa kukaribia kuwazidi kete Arsenal.
Wachezaji wengine waliokuwapo tayari kuingia Emirates ni kama Victor Wanyama
wa Celtic aliyekwenda Southampton kutokana na ubahili wa Arsenal,
Marouane Fellaini wa Everton, Michu wa Swansea na hata Ashley Williams
na Asmir Begovic.
Kila fursa inapotokea kwa Arsenal kuchukua wachezaji hao, wanajidai
wako bize na jambo jingine kisha akishachukuliwa au msimu wa usajili
ukiisha utasikia wakisema wamewakosa kwa bahati mbaya.
Msimu uliopita walisajili wachezaji wengi dakika za mwisho, wakiokota
wachezaji wa kweli na magarasa, na sasa muda unakatika kidogo kidogo,
tunaona Wenger akiwalaumu wanahabari eti kwamba wamepata walichotaka kwa
timu yake kuchabangwa na Villa. Sababu gani hii!
Kimsingi timu kama mabingwa watetezi, Manchester United, hawahitaji
kuongeza mchezaji, lakini wamehangaika vilivyo kumpata Cesc Fabregas,
Leighton Baines Marouane Fellaini japo wamekataliwa. Alex Ferguson kabla
ya kuondoka aliwapatia Wilfred Zaha na wanakataa kumwachia Rooney – wanacho kikosi kilichotwaa ubingwa na nyongeza ya Zaha.
Chelsea wamesheheni vipaji vingi, mchanganyiko wa chipukizi na
wakongwe lakini bado wameongeza wachezaji wapya. Manchester City
wamesajili fowadi kali kabisa, itakuwaje Arsenal waridhike wakati
hawakupata kuziba mapengo ya Patrice Vieira wala Robin van Persie?
Wenger anatamba na pauni milioni karibu 100 za usajili mfukoni, anaye Laurent Koscielny aliyezuiwa kucheza mechi baada ya kadi nyekundu, Bacary Sagna na Kieran Gibbs wakiuguliwa majeraha, bado anasema anawania taji?
Tatizo la Arsenal ni kwamba lazima wacheze vizuri sana kushinda mechi
zao, lakini waelewe tu kwamba United, Chelsea na City wanaweza kushinda
mechi hata wasipocheza vizuri, maana wachezaji wao wapo imara
kisaikolojia na wanahimili shinikizo.
Arsenal bado hawako hivyo, si ajabu hata nafasi ya nne wanayoililia
kila mwaka wakaikosa safari hii, maana wanatakiwa kununua aina ya
wachezaji wenye sifa kama wa timu hizo tatu, lakini Wenger anaonekana
kukwepa na kufikiri kivingine kabisa.
Bado Arsenal wanatakiwa kusajili mchezaji mmoja au wawili wa hadhi ya
juu, lakini kwa hali ilivyo, watabaki kuwajaribu chipukizi wao na
kujidai kwamba wanacho kikosi cha kufaa.
Wenger anatakiwa aelewe kwamba thamani haipo katika ile ada ya uhamisho, bali lile kabati lenye vikombe kila msimu unapomalizika. Yeye amehifadhi fedha miaka nenda rudi, na hiyo si kazi ya kocha.
Alichomoa kuwasajili Higuain na Gustavo kwa sababu ya fedha. Ni kweli
pauni zaidi ya milioni 30 ni nyingi kwa Higuain, lakini wanapokosa
mbadala wake maana yake ni majanga kwa klabu na safari nje ya nne bora
inaelekea kuanza mapema kabisa, isipokuwa kama watarekebisha mambo.
No comments:
Post a Comment